In Summary

Yanga ambayo iliwatumia mastaa wake kama, Mzambia Obrey Chirwa, Mzimbabwe Thaban Kamusoko, Kelvin Yondani 'Vidic' na Abdrew Vincent 'Dante', ilishindwa kuwapa raha mashabiki wake uliojitokeza kuipa sapoti kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wawakili pekee wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya
makundi, Yanga wameshindwa kutamba katika uwanja wake wa nyumbani baada ya kulazimishwa sare na Rayon Sports ya Rwanda.
Yanga ambayo iliwatumia mastaa wake kama, Mzambia Obrey Chirwa, Mzimbabwe Thaban Kamusoko, Kelvin Yondani 'Vidic' na Abdrew Vincent 'Dante', ilishindwa kuwapa raha mashabiki wake uliojitokeza kuipa sapoti kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Licha ya kufanya mashambulizi ya mara kwa mara, Yanga Wamejikuta wakigawana pointi 1-1 na Wanyarwanda hao na kuendelea kubaki mkiani kwenye kundi D ambalo linaongozwa na USM Alger ya Algeria yenye pointi 4, Gor Mahia ya Kenya pointi 2 ambazo ni sawa na za Rayon.
Ikicheza kwa nguvu na kufanya mashambulizi langoni mwa wapinzani wao, Yanga itajilaumu baada ya dakika ya 49 winga wake, Juma Mahadhi alishindwa kupasia mpira nyavuni baada ya shuti lake kuokolewa na mabeki wa Rayon huku ikikosa bao lingine dakika 68 kwa shuti la Chirwa kugonga mwamba na kuokolewa na mabeki wa Rayon.
Hata hivyo, mabadiliko ya Yanga kuwatoa Thaban Kamusoko nafasi yake ikachukuliwa na Raphael Daud, Chirwa aliyempisha Amiss Tambwe na baadaye Geofrey Mwashiuya ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Emmanuel Martin, hayakuweza kubadili matokeo ya mchezo huo.
Huo ni mchezo wa pili kwa Yanga baada ya ule wa kwanza waliocheza na USM Alger nchini Algeria wakapoteza kwa mabao 4-0.
Matokeo ya mchezo mwingine wa kundi hilo uliochezwa uwanjani Moi Kasarani, jijini Nairobi, Kenya Gor Mahia walishindwa kutumia vyema uwanja huo na kulazimishwa suluhu na Waarabu hao.
Huu ni mchezo wa nane kwa Yanga kushindwa kupata ushindi tangu kuondoka kwa kocha wake, George Lwandamina aliyetimkia kwao Zambia.
Kikosi cha Yanga kipa ni Youth Rostand, Hamis Ramadhan 'Kessy', Gadier Michael,
Kelvin Yondan 'Vidic,  Andrew Vincent 'Dante', Pius Buswita, Juma Mahadhi, Thaban Kamusoko/Raphael Daud, Obrey Chirwa/ Amiss Tambwe, Yusuph Mhiru na Geofrey Mwashiuya/ Emmanuel Martin.