In Summary
  • Yanga imezidi kujikita kieleni katika Ligi Kuu

Tanga. Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania si tu umeifanya Yanga izidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, pia umemaliza mkosi wa kutopata ushindi katika mechi tatu mfululizo.

Yanga jana ikiwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ilipata pointi tatu katika mchezo huo na kufikisha 58.

Awali, Yanga ilikuwa haijapata ushindi katika mechi tatu mfululizo ambazo ziliwapunguza kasi kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Nuksi ya Yanga ilianzia kwa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Stand United mkoani Shinyanga, ilitoka sare 1-1 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani Februari 3 kabla ya kutoka suluhu na Singida United, Jumanne iliyopita.

Yanga iliingia uwanjani kwa lengo moja tu la kutaka ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuikabili Simba, katika mchezo ujao utakaochezwa Jumamosi wiki hii.

Timu hiyo imeshusha presha ya mashabiki wake licha ya kupata ushindi mwembamba uliotokana na bao la dakika ya 26 lililofungwa na kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Bao la Feisal lilikuwa ni umaliziaji wa kazi nzuri iliyofanywa na beki wa kushoto wa Yanga, Gadiel Michael ambaye akiwa katika mazingira magumu alimtoka mlinzi mmoja wa JKT Tanzania na kupiga krosi iliyounganishwa kwa ustadi na kiungo huyo.

Kabla ya kuingia bao hilo, timu hizo zilishambuliana kwa zamu zikitumia zaidi mbinu ya kupigiana pasi ndefu, lakini safu zao za ulinzi kwa pande zote zilifanya kazi nzuri ya kuokoa hatari hizo.

Timu hizo zililazimika kutumia staili ya kupiga mipira mirefu ikionekana kama njia ya kukabiliana na mazingira ya uwanja wa Mkwakwani ambao eneo lake la kuchezea lilikuwa kavu na vichuguu vya hapa na pale ambavyo vilifanya mpira usitembee vizuri.

Ni Yanga ndio ilinufaika zaidi na mbinu hiyo kwani mashambulizi yake yalionekana kuitikisa safu ya ulinzi ya JKT Tanzania kulinganisha na wapinzani wao ambao washambuliaji wake Samuel Kamuntu na Ali Ahmed ‘Shiboli’ walishindwa kujipanga vizuri ndani ya eneo la hatari la Yanga.

Hata hivyo, ushindi huo haukupatikana kirahisi kwa kuwa baada ya kupata bao hilo Yanga lilazimika kufanya kazi ya ziada kuhimili vishindo vya mashambulizi ya JKT Tanzania ambayo ilibadilika na kutawala mchezo.

Miongoni mwa kazi nzuri iliyofanywa na safu ya ulinzi ya Yanga ilikuwa dakika ya 78 ambapo kipa Ramadhani Kabwili aliokoa shuti la Hassani Materema wakiwa wanatazamana ana kwa ana.

Yanga imefikisha pointi 58 baada ya kucheza michezo 23, ushindi ambao unawaweka katika hali nzuri kisaikolojia kuelekea mchezo dhidi ya watani wao wa jadi dhidi ya Simba.

Mchezo mwingine leo ilikuwa ni kati ya KMC ambayo iliyoialika Alliance FC kwenye Uwanja wa Uhuru iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Abdul Hillary alianza kuipatia KMC bao la utangulizi dakika ya 50 lakini dakika 14 baadaye beki Israel Patrick aliisawazishia Alliance.

Matokeo hayo yameisogeza Alliance hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 33 wakati KMC imepanda hadi nafasi ya nne ikiwa na pointi 36.