In Summary
  • Wezi wenye silaha wamtishia bastola na kumpora saa ya mkononi mshambuliaji wa Napoli, huku wakimtisha kwa kumwambia afunge bao katika mchezo ujao kwa ajili yao asipofanya hivyo watakua cha kumfanya

Naples, Italia. Wezi wenye silaha walimpora mshambuliaji wa Napoli ya Italia dakika chache baada ya kumalizika mechi Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool.

Polisi wamesema kuwa wezi hao walikuwa wawili walitumia pikipiki kulizuia gari la mchezaji huyo katikati ya barabara wakati akirejea nyumbani baada ya timu yake kuilaza Liverpool bao 1-0.

“Wezi hao waliokua na silaha walimtaka kutoa kila kitu cha thamani alichokuwa nacho lakini hakuwa na kitu chochote zaidi ya saa ya mkononi ambayo waliichukua,” ilisema taarifa ya polisi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa baada ya kuambulia saa pekee walimpa masharti kwamba katika mchezo ujao ahakikishe wanafunga bao kwa ajili yao kinyume cha hivyo watajua cha kumfanya.

“Walimpora saa aliyokuwa ameivaa aina ya Rolex Daytona watch, yenye thamani ya Pauni 18,000 na kumtaka afunge bao katika mchezo ujao kwa ajili yao kama anataka salama,”.

Mshambuliaji huyo anayepokea Pauni 45,000 kwa wiki alianza katika mchezo huo na kupumzishwa katika dakika ya 68 akimpisha Lorenzo Insigne aliyeifungia timu hiyo bao pekee katika dakika ya 90.

Polisi wameahidi kutumia kila wawezalo kuufutilia mbali mtandao huo wa wezi katika mji huo kwani wamekuwa wakiwalenga wachezaji kila mara.

Miongoni mwa wachezaji ambao wameshakutana na kadhia hiyo ni pamoja na Insigne, ambaye aliwahi kuporwa akiwa na mkewe kwenye gari mwaka 2013, wakati nahodha wa Napoli, Marek Hamsik pia aliwahi kuporwa akiwa na mkewe mwaka 2011.