In Summary
  • Lori la kampuni ya Zash Commercial Service African Limited lenye namba za usajili T 785 BQB lilikuwa likitokea Zambia kwenda Bandari ya Dar es Salaam limeacha njia ya kuingia daraja la Ubungo ambalo linajengwa

Dar es Salaam. Watu watatu wamenusurika katika ajali baada ya lori la kubeba mizigo kuacha njia na kuingia katika miundombinu ya daraja linalojengwa Ubungo Darajani jijini Dar es Salaam majira ya saa 5 usiku wa kuamkia leo Ijumaa. 

Lori hilo la kampuni ya Zash Commercial Service African Limited lenye namba za usajili T 785 BQB lilikuwa likitokea Zambia kwenda Bandari ya Dar es Salaam likiwa limebeba mchanga kutoka Congo tani 25 na watu watatu ndani yake ambao wote wametoka bila majeraha.

Baada ya kuacha njia, lori hilo liligonga uzio uliokuwa umewekwa na wakandarasi wanaojenga katika eneo hilo na kukwama katika mataruma ya vyuma vilivyolazwa katika daraja hilo jipya.

Akisimulia jinsi tukio hilo lilivyokuwa, msimamizi wa gari hilo, Mwalimu Shaibu amesema baada ya kuvuka mataa ya Ubungo wakiwa katika mwendo wa wastani walitahamaki kuona gari aina ya semi likiwa limeharibika mbele huku wakiwa wamekaribia kuligonga.

 "Walikuwa bado hawajaweka ishara kuwa gari hilo ni bovu, hivyo wakati tunajaribu kuhamia upande wa pili ili kulikwepa gari hilo tuligonga kingo za zege zilizowekwa katikati ya barabara gari ikayumba tukarudishwa upande huu hadi juu ya hili daraja linalojengwa."

"Baada ya gari kukwama na kuzima nilikaa kama dakika 15 nikisikilizia labda bado linaendelea kushuka maana nilijua tumekwisha. Baadaye niliposhuka na kuangalia sehemu nilipo nilihisi kizunguzungu kikali na sikuamini kama tumepona maana umbali kutoka tulipo na chini ni mkubwa," amesema Shaibu.

Pamoja na kunusurika katika ajali hiyo, Shaibu ameiomba Serikali kujaribu kuweka vizuizi visivyoweza kusababisha madhara hasa inapotokea dharura kama hiyo.

"Hata tusingekuja huku hayo mazege yangeweza kutuumiza pia kwa sababu ukiyagonga kwa nguvu yana athari," amesema Shaibu.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Jonas Kilowo ambaye ni mfanyabiashara katika eneo hilo amesema mazingira ya ajali yalivyokuwa wote waliamini hakuna atakayetoka mzima.

"Ilikuwa kama movie (picha ya video) jinsi dereva alivyokuwa anajitahidi kukwepa ajali hiyo, maana wangeigonga ile semi iliyokuwa imeharibika tungekuwa tunaongea mengine saa hizi," amesema Kilowo.