In Summary
  • Mshambuliaji huyo ameshindwa kusafiri na timu hiyo kwa madai ya kuugua

Awassa, Ethiopia. Pamoja na kushindwa kusafiri na timu mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajib amekuwa nguzo hapa Ethiopia.

Ajib ameshindwa kusafiri na Yanga ikielezwa ni mgonjwa, lakini tangu Yanga imetua mjini Awassa wanahabari mbalimbali wamefika hotelini na kutaka kufanya naye mahojiano.

Inaweza kukushangaza, lakini mchezo kwanza wa Yanga dhidi ya Welayta Dicha ulionyeshwa moja kwa moja hapa Ethiopia na kushudia jinsi Ajib alivyochangia ushindi huo wa mabao 2-0.

Kama haitoshi kocha wa Dicha, Ato Zenebe Fisseha alipofika hapa katika mahojiano na vyombo vya habari akimtaja Ajib kuwa ndiyo mtu aliyesababisha matokeo hayo ya mchezo wa kwanza.

Mmoja wa waandishi wa Televisheni ya Taifa, Muluken Ceedefaw amefika asubuhi ya leo katika hoteli ya Rori, Yanga ilipoweka kambi akitaka kufanya mahojiano na Ajib akitaja kuwa mshambuiaji huyo ndiye mtu tishio.

Hata hivyo, Ceedefaw hakuweza kufanikisha hilo baada ya kaimu kocha mkuu wa Yanga, Noel Mwandila kuzuia mahojiano hayo akiambiwa siyo muda muafaka, lakini hakujua kwamba Ajib hayupo kabisa na timu yake hapa.

Ceedefaw alisema Ajib wanamtambua kwa jezi namba 10 ni mtu hatari na anajua kuucheza mpira wachezaji ambao hapa Ethiopia wanakubalika kirahisi.

"Yule namba kumi ni mtu hatari kila shabiki hapa alipomuona alikubali uwezo wake, watu wengi wangefurahi kuona tumefanya naye mahojiano, lakini tumeambiwa hatutaweza kumpata labda baada ya mechi," alisema Ceedefaw.