In Summary

Leo Ijumaa Novemba 9, 2018, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amelieleza Bunge kwamba kesi 13 zimezofunguliwa kwenye mahakama mbalimbali za usuluhishi zenye jumla ya dola za Kimarekani 185,580,009.76

Dodoma. Tanzania inadaiwa Dola 185,580,009.76 (zaidi ya Sh400 bilioni) katika mashauri mbalimbali kwenye mahakama za kimataifa.

Hata hivyo. Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema mashauri yote yaliyopo kwenye mahakama hizo hayajatolewa uamuzi hivyo takwimu halisi za madai na gharama ambazo Serikali inaweza kuwajibika kulipa itapatikana baada ya mashauri kukamilika na uamuzi kutolewa.

Waziri Kabudi ametoa kauli hiyo bungeni Jijini Dodoma leo Ijumaa Novemba 9, 2018 wakati anajibu swali la Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe.

Zitto ameuliza Tanzania inakabiliwa na mashauri mbalimbali kwenye mahakama za kimataifa kama vile ICSID, ICA London, ICC Paris kuhusu masuala ya uwekezaji akahoji kuanzia Novemba 2015 mashauri hayo ni mangapi kwa idadi na kwenye mahakama zipi na jumla ya madai yote ni kiasi gani.

"Je, kuanzia mwaka 2008- 2018 kumekuwa na mashauri mangapi dhidi ya Jamhuri ya Muungano, mangapi yameamuliwa na Tanzania ilishinda mangapi," amehoji Zitto

Waziri Kabudi amesema mashauri yaliyofunguliwa kuanzia Novemba 2015 yapo 13 na yapo katika mahakama mbalimbali za usuluhishi ikiwemo permanent Court of Arbitration (PCA), London Court of International Arbitration (LCIA) na International Centre for settlement of Investment Dispute (ICSID) na huko Johannesburg Afrika Kusini kupitia Sekretarieti ya UNICTRAL.

“Jumla ya madai katika mashauri hayo ni dola za Kimarekani 185,580,009.76,” amesema Waziri Kabudi

Amesema kwa sasa hakuna kesi yoyote katika mahakama ya usuluhishi London iliyofunguliwa na kampuni ya Acacia Mining PLC shauri namba Arbitration UN 173686 na Shauri UN 1736867 yamefunguliwa Julai 3,2018 na makampuni ya Pangea Minerals Ltd na Bulyanhulu Gold Mining Ltd.

Mwisho,....