In Summary
  • Serengeti Boys, ambao wametoka kutwaa Ubingwa wa vijana wenye umri chini ya miaka 17 katika mashindano yaliyoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yaliyofanyika Burundi mwezi uliopita, wanajiandaa na mashindano ya Afrika kwa vijana wa umri huo yatakayofanyika mwakani hapa nchini.

Mwanza. Wizara ya Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo imesisitiza kuwa makosa ya kuwatelekeza vijana wa timu ya Taifa (U-17) ya Serengeti Boys iliyofuzu Fainali za Afrika mwaka jana hayatorudiwa tena.

Serengeti Boys, ambao wametoka kutwaa Ubingwa wa vijana wenye umri chini ya miaka 17 katika mashindano yaliyoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yaliyofanyika Burundi mwezi uliopita, wanajiandaa na mashindano ya Afrika kwa vijana wa umri huo yatakayofanyika mwakani hapa nchini.

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe alisema tofauti na ilivyojitokeza msimu uliopita, sasa watahakikisha wanawaandalia mazingira mazuri vijana waliopo kwenye kikosi hicho ili wawe na maisha mazuri hapo baadaye.

“Hawa vijana wametoka kutwaa Ubingwa wa Afrika Mashariki. Hatuwezi kukubali wapotee hivi hivi kama kipindi kilichopita. Mimi nitahakikisha angalau nawapeleka hata kwa Bakhresa awaajiri hata kwa kufuta rangi ukutani,”alisema Waziri Mwakyembe.

Alisema, kitendo cha kuteua vijana kwa maslahi ya Taifa kisha kuwaacha bila kujua hatma yao si jambo zuri kwani wachezaji hao wanafanya kazi nzuri ya kuitangaza nchi.

Kuelekea Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji mwakani, Waziri Mwakyembe alisema serikali imeandaa mkakati madhubuti kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuhakikisha Serengeti Boys inafanya vizuri.

“Tunaendelea kuwaandaa vyema vijana wetu wa Serengeti Boys na kwa bahati nzuri wanafanya vizuri jambo linalotufanya tuwe tunatembea kibabe. Tumejipanga kuwapeleka kambi nchini Sweden ili wakikutana na Waarabu pamoja na timu nyingine wawapige,”alisema Mwakyembe.