In Summary

Urafiki wa Florentino Perez na mshambuliaji huyo Mreno umefika mwisho, hata hivyo rais huyo atalazimika kutafuta mrithi wa nyota huyo wa zamani wa Manchester United haraka.

Madrid, Hispania. Real Madrid imekubali Cristiano Ronaldo ajiunge na Juventus, lakini sasa wanataka kujenga timu mpya hiyo ni wazi sasa watalazimika kusajili Galacticos wawili ili kulinda heshima ya klabu hiyo.

Urafiki wa Florentino Perez na mshambuliaji huyo Mreno umefika mwisho, hata hivyo rais huyo atalazimika kutafuta mrithi wa nyota huyo wa zamani wa Manchester United haraka.

Kila mmoja kuanzia mashabiki hadi viongozi wote wanasubiri kusikia kutoka kwa Perez atamsajili mshambuliaji gani mpya wa kuziba pengo la Ronaldo.

Real inaweza kufanikiwa bila ya Ronaldo, lakini ni wazi wanatakiwa kusajili mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao na kiwango kile alichokuwa akionyesha nyota huyo mwenye miaka 33.

Mpango wa klabu hiyo ni kusajili wachezaji wawili, iwe ni Galacticos au la lakini lazima wawili wasajiliwe.

Hakuna mchezaji mwenye kuhakikishia kuwa atafunga mabao 50, aliyokuwa akifunga Ronaldo.

 

Real Madrid ina fedha, lakini ni wachezaji wa aina gani wanataka kumsajili katika mazingira ya sasa na ugumu wake upo wapi.

Neymar ni chaguo la kwanza, lakini nyota huyo wa Brazili kuhamia Madrid inatakiwa nyota huyo wa zamani wa Barcelona anatakiwa kurudia kile alichokifanya Ronaldo kwa kuvunja ukaribu wake na Nasser Al-Khelaifi ili aweze kuachwa na mmiliki huyo wa Paris Saint-Germain.

Mshambuliaji Mfaransa Kylian Mbappe ni chaguo lingine, itakuwa vigumu kwao kumnasa si kwa sababu ya fedha bali ni malengo binafsi ya chipukizi huyo.

Mchezaji anayeweza kupatikana kwa haraka na wepesi ni Eden Hazard, nyota huyo wa Ubelgiji anaweza kujiunga na mabingwa hao wa Ulaya iwapo Chelsea watakuwa tayari kupokea dau la euro 100 milioni.

Pia, kuna wasiwasi kuhusu Harry Kane hasa kutokana na historia ya wachezaji wa England kushindwa kutamba katika LaLiga, pia kutakuwa na majadiliano makali na Daniel Levy kuhusu kumwachia nyota wake huyo.