In Summary
  • Rais  huyo wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwa mara ya kwanza kwenye  mchezo  wa Ligi Kuu,  utakaochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Klabu ya Simba inatarajiwa kukabidhiwa ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu wa 2017/2018  kwenye mchezo wa  Jumapili  dhidi ya Kagera Sugar na Rais Dk John Magufuli ambaye atakuwa mgeni rasmi katika mchezo huo.

Rais  huyo wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwa mara ya kwanza kwenye  mchezo  wa Ligi Kuu,  utakaochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya Yanga kupoteza mbele ya Tanzania Prisons, Mei 10 kwa mabao 2-0 kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

 

Akizungumzia kuwapo Dk Magufuli, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema kiongozi huyo wa nchi pia  atapokea  kombe kutoka kwa timu ya Taifa chini ya miaka 17 'Serengeti Boys'.

Serengeti Boys ilitwaa ubingwa wa kombe la Chalenji nchini Burundi ,  Aprili 29   baada ya kuifunga Somalia goli 2-0 kwenye mchezo wa fainali.

"Tumemuomba Rais awe mgeni rasmi katika kupokea kombe la Chalenji kutoka kwa vijana wetu wa Serengeti, lakini vile vile atawakibidhi kombe Simba.

"Hii itakuwa mara yake ya kwanza kufika uwanjani tangu awe Rais,  hivo ni jambo kubwa sana,  mpira ni moja ya viwanda na tukumbuke kwamba Rais wetu anataka uchumi wa viwanda," alisema Karia.

Karia aliongeza kwa kusema  wanaendelea na maandalizi ya mashindano ya Afcon kwa vijana yatakayofanyika 2019 kwa mara ya kwanza nchini.