In Summary
  • Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ inatarajiwa kuondoka leo usiku kwenda Cape Verde kucheza mchezo wa kufuzu fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani Cameroon.
  • Hata hivyo, Taifa Stars itaondoka na wachezaji watatu wa timu za Simba na Yanga waliopata majeraha wakati wakizitumikia klabu zao katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Dar es Salaam. Programu ya timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ imeanza kuleta kilio kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara zikihofia kuumia au kushuka ufanisi kwa nyota wao muhimu walioitwa kukitumikia kikosi hicho.

Taifa Stars inayojiandaa na mechi ya kufuzu Fainali za Afrika mwakani zitakazofanyika Cameroon, ilianza kambi Oktoba Mosi kujiandaa na mechi mbili za nyumbani na ugenini dhidi ya Cape Verde zitakazochezwa Oktoba 12 na 16.

Kutokana na ugumu na umuhimu wa mechi hizo, benchi la ufundi la Taifa Stars chini ya Kocha Emmanuel Amunike, liliomba wachezaji walioitwa katika kikosi hicho kutoka klabu za Ligi Kuu kuingia kambini mapema kupata maandalizi mazuri ya kiufundi kabla ya kuivaa Cape Verde.

Hata hivyo, Bodi ya Ligi ilitangaza uamuzi wa kuendelea na mechi za Ligi Kuu kama zilivyopangwa wakati kambi ya Taifa Stars ikiendelea.

Badala ya kuahirisha baadhi ya mechi za Ligi Kuu ili kutoa fursa kwa benchi la ufundi la Taifa Stars kupata muda wa kutosha wa maandalizi, bodi iliamua mechi za ligi kuendelea kuchezwa huku wachezaji wakiwekewa utaratibu wa kwenda kuzitumikia timu zao katika mechi zilizochezwa mwishoni mwa wiki na kurejea kwenye kambi ya Taifa Stars.

Uamuzi huo ulifanyika siku chache baada ya bodi hiyo kusogeza mbele mechi ya Simba dhidi ya Biashara United, Yanga na JKT Tanzania ili kuzipa nafasi za kujiandaa na mechi ya watani wa jadi iliyochezwa Septemba 30.

Kitendo cha kuwarudisha wachezaji kutumika katika timu zao na kurejea Taifa Stars, kimeibua hofu ya majeruhi jambo ambalo nusura lizigharimu Simba na Yanga ambazo zilicheza Jumamosi na Jumapili dhidi ya African Lyon na Mbao.

Katika mchezo dhidi ya African Lyon, nyota wawili wa Simba, Jonas Mkude na Shomari Kapombe walipata majeraha na siku moja baadaye Andrew Vincent ‘Dante’ na kipa Beno Kakolanya wa Yanga hawakumaliza mechi dhidi ya Mbao, baada ya kupata majeraha wakati Kelvin Yondani alimaliza licha ya kuumia.

Wachezaji wote watano walipata majeraha yanayofanana ambayo ni kubanwa na misuli, tatizo ambalo mara kwa mara linachangiwa na wachezaji kufanya mazoezi magumu.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema ameshangazwa na kitendo cha wachezaji kuwa na programu ya mazoezi mara mbili kwa siku.

“Simba inaweza kufanya vizuri bila uwepo wa wachezaji ambao wamekwenda kambi ya timu ya Taifa, lakini wasiwasi wangu ni programu ambazo wamekuwa wakifanya zinaweza kuchangia kuwaumiza au wakashindwa kuonyesha ufanisi.

Kwa kawaida mchezaji anapokuwa timu ya Taifa hapaswi kupewa mazoezi magumu, nashangaa wachezaji hapa wanafanya mazoezi mara mbili kwa siku asubuhi na jioni jambo ambalo lina athari kwa wachezaji, lakini kwa kipindi kama hiki hakuna kocha anayeweza kukubali kuwakosa wachezaji,” alisema Aussems.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila alisema aina ya majeraha ambayo wachezaji wamepata dhidi ya Mbao yana uhusiano na aina za programu wanayopata timu ya Taifa.

“Sipendi kuzungumzia programu za timu ya Taifa, lakini ukiangalia Dante na Kakolanya wote kwa pamoja wamepata majeraha ya kubanwa na misuli, hivyo unaweza kuona au kuhisi wanapewa mazoezi magumu,” alisema Mwandila.

Mkufunzi wa makocha Abdul Mingange alisema ingawa programu za timu ya Taifa zinaweza kuwa chanzo cha majeraha kwa wachezaji hao, zipo sababu nyingine zinazoweza kuwa chanzo.

“Sijahudhuria mazoezi ya Taifa Stars siwezi kutoa jibu la moja kwa moja kuwa programu zake ndio zimesababisha majeraha,” alisema Mingange.