In Summary
  • Timu za Simba na Asante Kotoko ya Ghana zilicheza mchezo wa sherehe ya Simba Day kwenye Uwanja wa Taifa.

Dar es Salaam. Simba inapaswa kumjenga kisaikolojia nyota mpya, Adam Salamba vinginevyo anaweza kupotezwa na mzimu wa penalti aliyokosa dhidi ya Asante Kotoko.

Timu hiyo juzi ililazimisha sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa kirafiki wa kuadhimisha Tamasha la ‘Simba Day’, uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Salamba alikosa penalti dakika ya 86, iliyodakwa kirahisi na kipa wa Kotoko, Felix Hannan. Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi Hans Mabena baada ya mshambuliaji huyo kuangushwa ndani ya 18 na beki, Amos Frimpong.

Mshambuliaji huyo ameanza kukabiliwa na presha baada ya kukosa penalti ambayo ingeipa Simba ushindi dhidi ya Asante Kotoko katika siku hiyo muhimu ambayo klabu hiyo imekuwa ikitumia kutambulisha nyota wake.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Salamba alisema jinamizi la penalti aliyokosa, linamvuruga kisaikolojia.

Mchezaji huyo aliyejiunga na Simba kutoka Lipuli ya Iringa alidai anahitaji mtaalamu wa saikolojia kumrudisha katika ubora wake katika soka.

Alisema baada ya kukosa penalti alikaribia kwenda kwenye benchi kumuomba kocha Patrick Aussems ampumzishe kwa kuwa tayari alikuwa ameathirika kisaikolojia.

“Kwa kweli nilitoka mchezoni. Niliwaharibia siku mashabiki waliojitokeza kwa wingi kutupa sapoti katika mchezo wetu huo ambao ulikuwa maalumu kwa ajili yetu na wao.

Naomba nitumie fursa hii kuwaomba radhi na kuwahakikishia kuwa sikukusudia kufanya hicho kilichotokea. Ilikuwa ni moja ya makosa yanayotokea mchezoni

“Sikuwa na mchezo mzuri baada ya kukosa penalti. Nilishukuru Mungu mwamuzi alipomaliza mpira nilikuwa nimevurugwa kisaikolojia ukizingatia idadi kubwa ya mashabiki waliojitokeza ndio nilichanganyikiwa kabisa,” alisema Salamba.

Aussems amemkingia kifua Salamba akisema tukio la kukosa penalti linaweza kumpata mchezaji yoyote.

“Mchezaji yeyote anaweza kukosa penalti, kikubwa anatakiwa kuwa mwangalifu na namna ya upigaji wa penalti lakini pamoja na yote alicheza vizuri,” alisema mbelgiji huyo.

Historia inaonyesha idadi kubwa ya wachezaji wa Simba na Yanga, ndoto zao za kutamba kwenye klabu hizo na soka la Tanzania zimekuwa zikiyeyuka kutokana na kukosa au kusababisha mikwaju ya penalti kwenye mechi muhimu ambazo mashabiki wa klabu hizo huwa na uhitaji mkubwa wa matokeo ya ushindi.

Presha huwa kubwa kwa wachezaji ambao hupoteza ama mikwaju ya penati au kufanya madhambi ambayo huchangia timu pinzani kuzawadiwa penalti.

Idadi kubwa ya wachezaji hujikuta wakiporomoka viwango kutokana na athari ya kisaikolojia inayosababishwa na presha au vitisho kutoka kwa mashabiki ingawa wachache wamefanikiwa kushinda vikwazo hivyo.

Baada ya kufanikiwa kuteka hisia za mashabiki wa Yanga kutokana na kiwango bora alichokuwa nacho kipindi hicho, beki David Mwakalebela alijikuta adui wa mashabiki wa timu hiyo baada ya kupoteza penalti dhidi ya Simba kwenye mchezo wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1992.

Mkasa kama huo ulimkuta beki Chibe Chibindu ambaye maisha yake Yanga yalikatishwa na penalti aliyokosa kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Tusker dhidi ya Simba ilyosababisha wapinzani wao kuibuka na ushindi wa penalti 5-4.

Mhanga mwingine wa penalti ni beki Novatus Lufunga ambaye alisababisha penalti kwenye mchezo dhidi ya Yanga, Februari 25, mwaka jana ambapo baada ya kosa hilo Simba ilimvumilia hadi mwishoni mwa msimu na kumtupia virago.

Baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kombe la FA ambalo alikuwa kipa bora Mghana Daniel Agyei aligeuka adui wa Simba hadi kutupiwa virago baada ya kukosa mkwaju wa penalti kwenye mchezo wa mtoano wa Kombe la SportPesa Super Cup dhidi ya Nakuru All Stars ya Kenya, mwaka jana.

Winga wa zamani wa Simba, Mrage Kabange alisema suala la Salamba kukosa penalti halipaswi kugeuka fimbo ya kumchapia mshambuliaji huyo chipukizi anayeinukia vyema.

“Sielewi kwa nini baadhi ya mashabiki wa Simba wanamlaumu Salamba kwa sababu suala la kukosa penalti ni kawaida na tumeona hata mastaa wakubwa duniani wamekuwa wakipoteza.

“Nafahamu presha itakuwa kubwa kwa upande wake lakini ninaamini kocha na benchi la ufundi litakuwa limejiandaa kumjenga kisaikolojia na kumrudisha sawa kiakili,” alisema.