In Summary
  • Mshambuliaji huyo anatakiwa kufunga mabao tisa ili kuifikia rekodi ya mkongwe huyo wa zamani wa Yanga

 Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi kesho anaanza kibarua kigumu cha kusaka mabao tisa katika mechi saba za Ligi Kuu ili kuvunja rekodi ya mabao 26 iliyodumu kwa miaka 19 ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’.

Wakati Simba ikiingia uwanjani kusaka pointi tatu muhimu dhidi ya Prisons ili kusogelea ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, Okwi atakuwa na changamoto nyingine ya kuhakikisha anafunga mabao ya kutosha ili ajitengenezee mazingira mazuri ya kuvunja rekodi iliyowashinda washambuliaji wenzake kwa miaka 19.

Mmachinga amemtabiria Okwi kuvunja rekodi hiyo msimu huu akisema ni mshambuliaji mzuri mwenye uchu wa mabao hivyo ana nafasi ya kuyafikia mabao yake.

“Ni mshambuliaji mzuri anayelijua goli na anaweza akaifikia rekodi yangu kwani bado ana nafasi kwa sababu ligi inaendelea na mechi bado nyingi hivyo kama akiendelea na kasi yake basi atavunja rekodi hii” alisema Mmachinga.

Okwi mwenye mabao 18 ameifikia rekodi ya Boniface Ambani wa Yanga aliyefunga mabao 18 msimu wa 2008/2009, Mussa Hassan Mgosi (Simba) aliyefunga mabao 18 msimu wa 2009/2010 na Mrisho Ngassa (Yanga) aliyefunga mabao 18 msimu wa 2010/2011.

Mshambuliaji huyo wa Simba anatakiwa kufunga bao moja kufikia rekodi za washambuliaji watatu waliofunga mabao 19 katika misimu tofauti ambao ni mshambuliaji wa Simba, Msomalia Isse Abushir msimu wa 2004/05, John Bocco (Azam) msimu wa 2011/12 na Amiss Tambwe (Simba) msimu wa 2013/14.

Mganda huyo anahitaji mabao mawili kuivunja rekodi ya mshambuliaji wa zamani wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma aliyefunga mabao 20 msimu wa 2005/06, endapo atafunga mabao tatu Okwi ataivunja rekodi wa 2015/16 ya mabao 21 iliyowekwa na Tambwe (Yanga).

Mshambuliaji huyo kipenzi cha mashabiki wa Simba, tayari amevunja rekodi ya mshambuliaji wa zamani wa Kagera Sugar, Michael Katende aliyefunga mabao 11 msimu wa 2007/2008, Kipre Tchetche (Azam) aliyefunga mabao 17 msimu wa 2012/2013, Saimon Msuva (Yanga) mabao 17 msimu wa 2014/ 2015 na Saimon Msuva (Yanga) na Abdulraham Mussa(Ruvu Shooting) waliofunga mabao 14 kila mmoja msimu uliopita.

Okwi katika mechi saba zilizobaki anatakiwa kufunga mabao tisa yatakayomfanya afikishe jumla ya mabao 27, ili kuivunja rekodi ya Mmachinga, lakini iwapo atafunga mabao nane katika mechi saba zilizobakia kabla ya ligi kumalizika, yatamfanya afikie mabao 25 ingawa hatoivunja.

Ukiondoa mechi dhidi ya Prisons kesho, Simba itakabiliana na timu za Lipuli, Yanga, Ndanda FC, Kagera Sugar, Singida United na kufunga hesabu na Majimaji.

Wakati ugumu wa mechi ya Yanga unatokana na wapinzani wao katika mbio za kusaka ubingwa, ugumu wa mechi dhidi ya timu za Prisons na Singida United utachangiwa na ushindani wa timu hizo kuwania kumaliza katika nafasi tatu za juu katika msimamo wa ligi wakati michezo dhidi ya timu za Lipuli, Kagera Sugar, Ndanda FC na Majimaji, ugumu wake utachangiwa na vita inayozikabili timu hizo kujinasua katika janga la kushuka daraja.

Okwi anaweza kuivunja rekodi hiyo kwani licha ya umahiri wake katika kufumania nyavu msimu huu, amekuwa na bahati ya kufunga idadi kubwa ya mabao katika mechi ambazo Simba inacheza jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hizo saba ambazo Simba imebakiza kabla ya ligi kumalizika, michezo minne dhidi ya Prisons, Yanga, Ndanda na Kagera itacheza Dar es Salaam wakati mitatu itakayokabiliana na dhidi ya Lipuli, Singida United na Majimaji, itakuwa ugenini.

Mbali na hilo, Okwi pia atakuwa anasaka rekodi ya kuzifunga timu 14 kati ya 16 zinazoshiriki Ligi Kuu msimu huu kwani hadi sasa ameshafumania nyavu dhidi ya timu tisa na bado hajazifunga, Yanga, Prisons, Kagera Sugar, Ndanda, Lipuli na Stand United.

Mshambuliaji huyo alisema anatamani kuona anaibuka mfungaji Bora wa Ligi Kuu msimu huu ingawa ndoto yake ya kwanza ni kuisaidia Simba kutwaa Ubingwa.

“Jambo la kwanza ni kuisaidia timu yangu kutimiza lengo la kuchukua ubingwa, lakini nitafurahi zaidi kama tutakuwa mabingwa huku nikiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu,” alisema Okwi.

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema upo uwezekano mkubwa kwa Okwi kuifikia na kuivunja rekodi ya Mmachinga.

“Kinachoniaminisha Okwi anaweza kufikia na kuvunja rekodi hiyo, ni kwamba kati ya mechi walizobakiza, nne watacheza kwenye Uwanja wa Taifa ambako Okwi amekuwa akifanya vizuri na kufunga mabao mengi kutokana na ubora wa kiwanja. Lakini mwisho wa siku hilo litatimia iwapo atakuwa fiti katika mechi hizo zilizobakia,” alisema Mayay.