Dar es Salaam. Mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame, Azam FC wamefurahi kupata nafasi ya kutetea taji lao dhidi ya Simba hapo kesho Ijumaa.

Azam FC imefuzu kwa fainali ya Kombe la Kagame baada ya kuichapa Gor Mahia kwa mabao 2-0, wakati Simba ikishinda bao 1-0 dhidi ya JKU katika mechi za nusu fainali.

Mshambuliaji wa Azam, Mbaraka Yusuph amesema hatua waliofika ni nzuri na imewapa nguvu kubwa ya kuendelea kupigania kubakisha kombe hilo.

"Kama tumeweza kufika hapa, basi hatua iliyobaki hakiwezi kushindikana kitu, kikubwa tunatakiwa kupambana kadri tutakavyoweza ili kuweka rekodi ya aina yake,"alisema Mbaraka.

“Simba ni timu ngumu, lakini itawafanya wadhihirishe uwezo wao kwamba hawajafika fainali hiyo kwa bahati mbaya. Tunacheza na timu yenye ushindani mkali, hivyo itakuwa mechi ngumu."

Kiungo Joseph Kimwaga amejipa asilimia 90 za kubakisha taji hilo, akidai 10 ni zile za ushindani dhidi ya Simba wanayocheza nayo fainali hizo.

"Mafanikio yanakuja kwa kujituma, nidhamu na kujiamini na ndio maana naamini tuna asilimia 90 ya kubakiza kombe hilo, huku asilimia zilizobaki ni za kutoidharau Simba ambao ina nyota wanaojua kupambana,"alisema Kimwaga.