In Summary

TImu zinazofuzu kwa 16 bora kila moja ipewa fedha na chakula kwa watu 32.

 Msimu wa tano wa mashindano ya soka yanayoshirikisha timu za mtaani 'Ndondo Cup' umezinduliwa rasmi leo huku yakitarajiwa kushirikisha jumla ya timu 64 kutoka mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

Kati ya timu hizo 64, 48 zitaanzia hatua ya awali ambayo itachezwa kwa mtindo wa mtoano kusaka timu 32 zitakazopangwa katika makundi nane yenye timu nne kila moja na baada ya hapo timu mbili zitakazoshika nafasi za juu kwa kila kundi zitaingia hatua ya 16 bora.

Mwenyekiti wa kamati ya kuratibu mashindano hayo, Shaffih Dauda alisema kutokana na umuhimu na mvuto ambao mashindano hayo yamekuwa nayo tangu yalipoanzishwa mwaka 2014, safari hii wameyaboresha ili yawe chachu zaidi ya kukuza na kuinua mpira wa miguu.

"Miongoni mwa maboresho ambayo yamefanyika ni kutoa fedha za maandalizi kwa timu kuanzia hatua ya 16 Bora hadi zile zitakaozofuzu fainali, lakini pamoja na hilo, tutatoa usafiri na chakula kwa watu wasiozidi 32 kwa kila timu ambayo itafanikia kufuzu hatua hiyo na kuendelea," alisema Dauda.

Wakati huohuo; Tofauti na mashindano yaliyopita, awamu hii Ndondo Cup itaambatana na mashindano ya vijana wenye umri usiozidi miaka 15 kwa vituo, shule na timu za vijana wadogo hapa jijini yatakayojulikana kwa jina la 'Ndondo Academy'.

"Sisi kama Chama Cha Mpira wa Miguu mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) tunaamini kwamba soka la vijana wadogo ndio msingi mkuu wa maendeleo ya mpira wa miguu hivyo tumekuja na programu hii tukiamini kwamba itasadia kutupatia vijana watakaokuja kulisaidia Taifa letu kisoka siku za usoni," alisema Mwenyekiti wa DRFA, Almas Kasongo.

Mashindano hayo ya mwaka huu yamedhaminiwa na kampuni za mChEZA,Shadaka Sports, Azam Media na Macron