In Summary
  • Mwadui inayoshika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi, ina pointi 30 ambazo hazitofikiwa na timu za Ndanda FC na Njombe Mji zilizopo mkiani mwa msimamo wa ligi, lakini Bizimungu ambaye ni raia wa Rwanda ametamba kuwa uhakika wa kubaki Ligi Kuu haufanyi wasitamani kushinda dhidi ya Yanga.

Dar es Salaam. Licha ya Mwadui FC kubaki Ligi Kuu, kocha wa timu hiyo Ally Bizimungu ameitangazia vita Yanga, akidai haitokuwa salama watakapokutana Mei 19, mkoani Shinyanga.

Mwadui inayoshika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi, ina pointi 30 ambazo hazitofikiwa na timu za Ndanda FC na Njombe Mji zilizopo mkiani mwa msimamo wa ligi, lakini Bizimungu ambaye ni raia wa Rwanda ametamba kuwa uhakika wa kubaki Ligi Kuu haufanyi wasitamani kushinda dhidi ya Yanga.

Bizimungu alisema amepanga kupata ushindi kwenye mchezo huo, ili kutanua pengo la pointi dhidi ya timu zilizo mkiani kama njia ya kuonyesha ubora kati ya Mwadui na timu za mkiani.

“Mechi yetu na Yanga ndio itakayotutofautisha na wapinzani wangu ambao wengi wapo kwenye hatari ya kushuka. Ntakipanga kikosi changu kuhakikisha kinafanya kitu cha tofauti katika mchezo huo,

“Nimewaambia wachezaji wangu kwamba hiyo ni mechi ya kuonyesha wao ni akina nani. Ili waweze kusajiliwa na kuzitumikia klabu kongwe za Simba na Yanga kama wengi wanavyotamani, ni lazima wazifunge la sivyo wakicheza kilegevu wataonekana thamani yao ndogo,” alisema Bizimungu.