Dar es Salaam.Mchezaji nyota wa kimataifa, Saimon Msuva amemtaka Ibrahim Ajibu wa Yanga kuzingatia mambo matatu katika maisha yake mapya katika Klabu ya TP Mazembe Englebert ya DR Congo.

Ajibu aliyefunga mabao saba na kutoa usaidizi wa pasi 16 zilizozaa mabao, anatarajiwa kujiunga na TP Mazembe, baada ya kumalizika msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Msuva anayetarajiwa kuwasili nchini leo kwa Ndege ya Emirates akitokea Morocco anakocheza soka ya kulipwa Difaa El Jadida, amemtaka Ajibu kuzingatia nidhamu, uvumilivu na kujituma uwanjani.

Nyota huyo alisema Ajibu ni mchezaji mwenye kipaji cha soka, lakini anatakiwa kulinda nidhamu ndani na nje ya uwanja na asibweteke na mafanikio aliyopata ya kutua TP Mazembe.

“Hakuna maisha magumu kama kuishi mbali na nyumbani, nilivyopata nafasi ya kujiunga na Difaa niliamua nitakabiliana na jambo lolote. Ugumu wa maisha ya Morocco ulianzia katika hali ya hewa (baridi), mawasiliano, muda mrefu wanazungumza kiarabu,” alisema Msuva.

Msuva alisema nje hakuna maisha ya posho kama Bongo ambayo yapo katika klabu nyingi, hivyo Ajibu anatakiwa kuwa makini na jambo hilo ili kulinda heshima yake.

Naye Rashid Mandawa anayecheza soka ya kulipwa BDF XI ya Botswana, alimtaka Ajibu kuvumilia changamoto zote ambazo atakutana nazo akiwa DR Congo.

“Maisha ya wachezaji wa Tanzania ukiwa nje yanafanana, unapotoka ni kama anaanza moja. Ajibu anatakiwa kukubaliana na kile ambacho atakumbana nacho DR Congo,” alisema Mandawa.

Naye winga wa OC Bukavu Dawa ya DR Congo, Selemani Kassim ‘Selembe’ ambaye ameipandisha Ligi Kuu timu hiyo, alisema kinachoweza kumfanya Ajibu awe na thamani akiwa DR Congo ni ubora wa kiwango chake cha uchezaji.

Selembe ambaye alitamba Tanzania Bara akiwa Stand United na timu ya Taifa ya Zanzibar, ‘Zanzibar Heroes’ alisema anatambua uwezo wa Ajibu anachotakiwa kufanya ni kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake TP Mazembe.