In Summary
  • Bondia huyo ameshinda pambano lake la TKO baada ya kumtandika mpinzani wake ngumi 96 katika raundi mbili

Dar es Salaam. Bondia Hassan Mwakinyo ametua Dar es Salaam alfajiri ya leo na kuungana na familia yake kwenda Bungeni Dodoma huku akiweka wazi lengo lake kwa sasa ni kuzichapa na Amir Khan.

Mwakinyo amerejea alfajiri (Ijumaa) kwa ndege ya Oman Air akitokea nchini England alipomchapa bondia wa Uingereza, Sam Eggington kwa TKO katika raundi ya pili kwenye pambano la raundi kumi lenye uzito wa Super Welter lililokuwa la utangulizi kabla ya kupanda Amir Khan aliyezichapana na Sam Vargas.

Akizungumza baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Mwakinyo alisema anamtamani kupambana na bondia Khan.

“Sisi wote ni watu unajua kwamba unaweza ukaona mtu jina lake lipo katika kiwango cha juu, lakini inakuwa tofauti na unavyokutana naye uwanjani, kwahiyo natamani nicheze hata na Khan,” alisema Mwakinyo.

Bondia huyo amewaomba Watanzania waendelee kumpa sapoti ili aendele kufanya mazoezi kwa juhudi ili kuipeperusha vema bendera ya Tanzania.

 

AZUNGUMZIA USHINDI WAKE

Baada ya kufanikiwa kushinda kutokana na kumtandika mpinzani wake ngumi 96 ambazo 51 kati ya hizo alipiga raundi ya pili, alisema ushindi huo haukuwa mwepesi hata kidogo.

“Haikuwa kazi rahisi hata kidogo kiukweli kwa sababu na yeye alikuwa yupo fiti, lakini nilijitahidi kupambana na kuhakikisha natoka na ushindi katika pambano lile kwani ndio lililkuwa lengo kuu.”

Aliongeza katika mchezo wa ngumi hata uwe bingwa vipi kama ngumi ni kali hauwezi kuivumilia itafika muda lazima utakubali tu.

“Hauwezi kuzoea ngumi hata kidogo na hiyo kwa mtu yeyote kwahiyo naweza kusema kwamba nilitumia nafasi yangu vizuri pale ambapo nilipata nguvu ya kupiga,” alisema Mwakinyo.

 

AONA MWANGA MBELE

Mwakinyo anasema ushindi huo umempa mwanga wa kufanya vizuri zaidi kuelekea kutimiza malengo yake katika mchezo huo.

“Huu ushindi ni kama umenipa chachu mimi ya kufanya mazoezi zaidi ili niwe vizuri, kuna vitu ambavyo nimejifunza nikiwa kule kwa hiyo nasema bado nina kiu kubwa,” alisema Mwakinyo.

Bondia huyo aliongeza hakuna kitu kikubwa au siri ya kufanya vizuri zaidi ya kufanya mazoezi na kujitunza kuhakikisha anakuwa fiti muda wote.