In Summary
  • Yanga imepania kuweka heshima CAF baada ya kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu

Dar es Salaam. Achana na matokeo ya kupoteza mechi tatu za Ligi Kuu Bara, Yanga inaingia kwenye Uwanja wa Taifa kesho kuwavaa Rayon Sport ya Rwanda katika mchezo wa pili wa Makundi, Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ikiwa kivingine kabisa.

Timu hiyo iliyoanza vibaya kwa kufungwa mabao 4-0 na USM Alger, Mkwasa alisema kuwa wachezaji wake wameiva vizuri na ndiyo maana wamejiandaa kikamilifu.

“Najua watu watasema Yanga imefungwa, sisi tulikuwa na plan zetu, plan A ilikuwa Ligi Kuu na baada ya kukosa huko tumeweka mkazo kwenye plan B, mechi za kimataifa.

“Watu wanatushangaa kupeleka wachezaji 13 Mbeya sawa tumefungwa, tumefungwa pia Morogoro, lakini tuko kimkakati zaidi. Achana na hayo, mkakati hapa ni kufika mbali Kombe la Shirikisho.

“Utaelekeza vipi nguvu mechi za ligi wakati ni kukamilisha ratiba, unaweza kuumiza wachezaji, ndiyo maana majembe tuliyaacha Dar kujipanga kwa ajili ya Rayon na wengine wakaenda kucheza Mbeya na Morogoro.”

Mkwasa alisema wana imani watafanya vizuri kwenye mchezo huo ambao endapo Yanga itashinda, itajiweka katika nafasi nzuri kwenye Kundi D linaoongozwa na USM Alger ya Algeria yenye pointi tatu, Gor Mahia ya Kenya na Rayon zenye pointi moja kila moja.

“Tunawaambia mashabiki wetu waje uwanjani, vijana wako na ari, tumejipanga kushinda, tunajua ni mchezo mgumu lakini tunataka kuweka heshima pia kushinda nyumbani ili kujiweka katika nafasi nzuri,” alisema Mkwasa.

KIKOSI CHA YANGA

Habari njema kwa mabingwa hao wa msimu uliopita ni kuwepo kwa nyota wake wote wa kikosi cha kwanza kwenye mchezo wa Kesho.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Dismas Ten alisema kwenye mchezo wa kesho watawatumia wachezaji wake wote ikiwamo wale ambao hawakusafiri na timu nchini Algeria kwenye mchezo wa kwanza wa makundi.

Wachezaji ambao hawakusafiri na timu ni Ibrahim Ajibu, Kelvin Yondani, Obrey Chirwa, Thabani Kamsoko na Pappy Kabamba.

“Wote watakuwepo, kucheza ama kutokucheza itategemea na mipango ya kocha lakini wote wako timamu na timu, mchezaji ambaye atakosekana ni Juma Makapu,” alisema.

Kocha wa timu hiyo, Mwinyi Zahera alisema timu iko katika ari ya ushindi na wanachokifikiria ni kushinda mchezo huo na mingine ya makundi ili kusonga mbele.

“Nafasi tuliyobaki nayo ni hii ya CAF, lazima tupambane, tunachokihitaji ni kuweka heshima kimataifa na ili tufike huko ni kupambana kwenye mechi zetu za nyumbani na tutaanza na Rayon,” alisema.

Kocha huyo alisema ameshawasoka kwani amewanasa Wanyarwanda hao, baada ya kuwasaka na kuipata mikanda mitatu ya mechi zao katika Kombe la Shirikisho Afrika, Rayon Sport na kukiri kwamba ni wazuri, lakini wanafungika.

Zahera alikaririwa na Gazeti la Mwanaspoti juzi akisema tayari ameinasa mikanda mitatu ya Rayon ikiwemo ya mechi zake mbili za ligi na moja ya Kimataifa wakati wakipambana na Gor Mahia na kujua kila kitu kuhusu wapinzani wao hao.

Zahera alisema Rayon sio timu nyepesi akibaini wako vizuri kwa stamina na pia ina watu wanaojua kuamua mechi. Baada ya kutazama mechi hizo kwa kina amewataka wachezaji wake kutambua kuwa Wanyarwanda hao siyo watu wa kupuuza. Alisema safu ya ushambuliaji ya Rayon ina ubora mzuri kwa kuwa na washambuliaji wenye uwezo na mikanda hiyo imempa akili ya kujua aitengeneze vipi timu yake. “Rayon sio timu tunayotakiwa kuidharau wana ubora wao lakini hata sisi Yanga tuna ubora wetu,nimepata picha nzuri sasa najua ni aina gani ya maandalizi tunatakiwa kukazania tukiwa mazoezini.”

Beki wa klabu hiyo, Andrew Vincent ‘Dante’ alisema kuelekea katika mchezo huo akirejea Kelvin Yondani, kutaongeza umakini katika safu ya ulinzi hali ambayo itakuwa ngumu kuwaruhusu Rayon kuwasogelea.

“Ninja ni mzuri lakini bado anahitaji uzoefu, mimi mwenyewe sio mzoefu sana lakini tunapocheza sisi wawili wote hatuna uzoefu inakuwa tabu kidogo, Yondani akiwepo kunakuwa kumetulia pale nyuma na kazi inakuwa sio kubwa sana,” alisema.

Naye Emmanuel Martin aliyekuwa kikosi kilichokuwa Morogoro, alisema mechi hiyo ina umuhimu kwao ndio maana waligawanywa vikosi viwili kuelekea mchezo huo.