In Summary
  • Timu 10 ambazo hazijui hatma yao katika Ligi Kuu Bara hadi sasa ni Ruvu Shooting yenye pointi 29, Lipuli (28), Mwadui (26), Mbeya City (26), Stand United (25), Kagera Sugar (24), Ndanda (23), Mbao (23), Majimaji (19) na Njombe Mji (18).

 Zimebaki mechi sita tu zakuamua timu mbili za kushuka daraja kati ya 10 zinapumulia mashine zikitakiwa kupambana na hali zao ili  kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

Timu 10 ambazo hazijui hatma yao katika Ligi Kuu Bara hadi sasa ni Ruvu Shooting yenye pointi 29, Lipuli (28), Mwadui (26), Mbeya City (26), Stand United (25), Kagera Sugar (24), Ndanda (23), Mbao (23), Majimaji (19) na Njombe Mji (18).

Vumbi la Ligi Kuu litatimka leo kwenye viwanja vinne kwa Lipuli kuivaa Singida United kwenye Uwanja wa Samora Iringa, huku Mwadui itawakaribisha Stand United kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga wakati Mbao watakuwa wenyeji wa Majimaji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mechi ya Azam dhidi ya Njombe Mji ipo katika hatihati ya kufanyika baada ya matajiri hao Chamanzi kuomba isogezwe mbele baada ya kucheza mechi juzi Ijumaa dhidi ya Ruvu Shooting na kupigwa 2-0.

Timu zenye wakati mgumu zaidi ni Ruvu Shooting, Mwadui, Stand United, Kagera Sugar, Ndanda na Mbao ambazo karibu mechi tano kati ya sita wanakutana wenyewe kwa wenyewe walio katika hatari ya kushuka daraja hivyo kuzifanya mechi hizo kuwa ngumu.

Lipuli na Mbeya City zinaweza kupata ahueni kwani katika michezo sita waliyobaki nayo, minne wanakutana na timu ambazo ziko juu kwenye msimamo na hazina presha ya kushuka daraja lakini zikiwa na presha ya ubingwa.

Lipuli inahitaji kushinda michezo mitatu tu ili kujihakikishia nafasi ya kubaki kwenye ligi msimu ujao kwani itakuwa imefikisha pointi 37.

Mwadui yenye pointi 26 inahitaji kukusanya pointi 10 katika michezo yake sita iliyobaki kama ilivyo kwa Mbeya City ili kuwahakikishia usalama wa kubaki kwenye ligi msimu ujao.

Stand United, Kagera Sugar, Ndanda na Mbao zenyewe zinahitaji kushinda michezo minne tu ili ziwe salama wakati Majimaji na Njombe Mji ndizo zina kazi zaidi kwani zinatakiwa zisipoteze mchezo wowote katika sita iliyobaki.

Kocha wa Majimaji, Habib Kondo alisema anajua wana kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha wanabaki ligi msimu ujao, lakini kwenye soka lolote linaweza kutokea.

“Tuko katika hali mbaya lakini tutajaribu kuendelea kupambana ili tujue mwisho tutakuwa wapi. Soka ni mchezo wa maajabu, unaweza ukadhani fulani atashuka na akaja kushuka mwingine, hivyo muhimu ni kuongeza juhudi katika michezo yetu ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,”alisema Kondo.