In Summary
  • Mbali na Aveva, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Zacharia Hanspoppe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba na mfanyabiashara, Franklin Lauwo, ambao mpaka sasa bado hawajakamatwa.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa siku kumi kwa upande wa Mashtaka kufanya marekebisho katika hati ya mashtaka, katika kesi ya kula njama na kughushi, inayowakabili, vigogo wa Simba akiwemo Rais wake, Evans Aveva na Makamu, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ ili kesi ya msingi iweze kuendelea.

Mbali na Aveva, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Zacharia Hanspoppe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba na mfanyabiashara, Franklin Lauwo, ambao mpaka sasa bado hawajakamatwa.

Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya kupitia maombi ya upande wa utetezi waliyowasilisha mahakamani hapo, wakiomba mahakama hiyo, itoe amri ya kuwaondoa katika hati ya mashtaka, mshtakiwa Hanspoppe na Lauwo, ambao hawajakamatwa.

Akisoma uamuzi huo, Hakimu Simba alisema anakubaliana na hoja za upande wa utetezi kuwa mahakama itaendelea kuwasubiri washtakiwa hao ambao hawajakamatwa mpaka lini wakati kesi dhidi ya wateja wao ikiwa imesimama.

“Mahakama imepitia kwa makini hoja za pande zote na kwamba imekubaliana na hoja za upande wa utetezi kuwa mahakama itaendelea kuwasubiri washtakiwa ambao hawajakamatwa hadi lini? “ alisema na kuongeza

“Kwa sababu hizi, mahakama imetoa amri kwa upande wa mashtaka kufanya marekebisho katika hati ya mashtaka au imuondoe mshtakiwa wa tatu na wa nne katika hati hiyo ya mashtaka, ili kesi iweze kuendelea kwa washtakiwa wawili ambao wapo mahakamani, kwa sababu nao wana haki zao” alisema Hakimu Simba.

Hakimu Simba alisisitiza endapo upande wa mashtaka watashindwa kutekeleza amri hiyo, mahakama hiyo itatoa amri nyingine.

Baada ya Maelezo hayo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 21, itakapotajwa na upelelezi wa shauri hilo umeshakamilika.

Awali, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai, ulidai kuwa shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya uamuzi na wapo tayari kusikiliza.

Hata hivyo, wakati uamuzi huo unatolewa, mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Aveva, hakuweza kuletwa Mahakamani kwa sababu ni mgonjwa.

Mei 14, mwaka huu, mawakili wa Aveva na Kaburu , Nehemia Nkoko na Timotheo Wandiba, waliiomba mahakama itoe amri ya kuwaondo washtakiwa Hanspoppe na Lauwo ambao hawajakamatwa au kubadilisha hati ya mashtaka ili waendelee na usikilizwaji wa mashtaka dhidi ya wateja wao ambao tayari wameshasomewa mashtaka.

Wakili Wandiba alihoji kuwa mahakama itaendelea kuwasubiri washtakiwa hao ambao hawajakamatwa hadi lini wakati kesi dhidi ya wateja wao ikiwa imesimama?

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka kumi likiwemo la kula njama, matumizi mabaya na kughushi nyaraka.