Dar es Salaam.Safu ya ulinzi ya Simba imeshikilia hatima ya timu hiyo katika mechi yake ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho.

Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa haina presha kubwa kwa safu yake ya ushambuliaji ingawa haijapata bao katika mechi mbili mfululizo zilizopita dhidi ya AS Vita na Al Ahly kutokana na rekodi nzuri ya kufunga mabao inapocheza nyumbani.

Hata hivyo, idara ya ulinzi ya Simba imeonekana kuyumba na kuvurunda mara kwa mara pasipo kuonyesha kuimarika jambo linalowapa faida wapinzani wao kufunga mabao ambayo yamekuwa yakiwagharimu.

Kufanya vibaya kwa safu ya ulinzi katika siku za hivi karibuni, kunaiweka Simba kwenye wasiwasi mkubwa kwa kuwa inalazimika kushinda ili kuweka hai matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Takwimu za mechi tano zilizopita ambazo Simba ilicheza katika mashindano mbalimbali zinaonyesha safu ya ulinzi imeruhusu wastani wa mabao mawili katika kila mchezo.

Katika mechi tano za mwisho kabla ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui FC, nyavu za Simba zimetikiswa mara 13 ikiwa ni sawa na wastani wa mabao 2.6 kwa kila mchezo.

Simba iliruhusu mabao 10 katika mechi mbili katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita na Al Ahly. Katika Kombe la SportPesa ilifungwa mabao matatu kwenye mechi tatu dhidi ya AFC Leopards, Bandari FC na Mbao FC.

Changamoto kubwa inayoonekana kuigharimu safu ya ulinzi ya Simba ni kumkosa beki kiraka Erasto Nyoni ambaye alipata majeraha katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Nyoni ni mhimili wa safu ya ulinzi kutokana na utulivu, uwezo wa kuwapanga mabeki wenzake na kusawazisha makosa yao pale wanaposhambuliwa tofauti na sasa ambapo Simba imekosa kiongozi wa namna hiyo.

Kwa kudhihirisha pengo la Nyoni limeitesa Simba, katika mechi 10 ambazo hajacheza, timu hiyo imefungwa mabao 15. Simba haina presha na safu ya ushambuliaji ambayo pamoja na kutofanya vizuri ugenini, imekuwa na rekodi inayovutia inapocheza Uwanja wa Taifa.

Katika mechi tano za mwisho za mashindano ya kimataifa Simba imefunga mabao 16.

Kocha wa Mbao FC, Ally Bushiri alisema Simba inaruhusu idadi kubwa ya mabao kutokana na kukosa umakini.

“Simba huwa hawako makini pindi wanapokuwa na mpira, lakini pale wanapopoteza hawapambani kutafuta na kupora kutoka kwa wapinzani sasa wanapokutana na timu zinazojua kuchezea mpira inajikuta ikifungwa mabao mara kwa mara,”alisema Bushiri.

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema safu ya ulinzi ya Simba imekuwa haina mawasiliano mazuri.

“Ukiangalia aina ya mabao wanayofungwa ni matokeo ya mabeki kukosa mawasiliano, pia wamekuwa wakifanya makosa binafsi sasa wanapokutana na timu za wachezaji wa daraja la juu, wanajikuta wanaadhibiwa kwa kila kosa wanalofanya,” alisema Mayay.