In Summary
  • Akizungumza na Mwanaspoti, kwenye Uwanja wa Camp Toyoyo, mapema leo, Mfaransa huyo alisema kukosekana kwa wachezaji wa Kogalo katika orodha ya wachezaji 27 aliowaita kwa ajili ya majaribio, kabla ya kupata kikosi cha kwanza cha Stars, kunatokana na timu hiyo kukabiliwa majukumu mengine ya kuwakilisha nchi

Kocha wa Harambee Stars, Mfaransa Sebastien Migne, amezima minong'ono iliyoaza kusambaa kwamba ameamua kuwafungia vioo wachezaji wa Gor Mahia katika kikosi chake kwa kusisitiza hatacha mchezaji yeyote mwenye kipaji.

Akizungumza na Mwanaspoti, kwenye Uwanja wa Camp Toyoyo, mapema leo, Mfaransa huyo alisema kukosekana kwa wachezaji wa Kogalo katika orodha ya wachezaji 27 aliowaita kwa ajili ya majaribio, kabla ya kupata kikosi cha kwanza cha Stars, kunatokana na timu hiyo kukabiliwa majukumu mengine ya kuwakilisha nchi.

Migne alisema baada ya kumalizika kwa mchezo wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Afrika, kati ya mabingwa hao mara 16 wa soka nchini na USM Algiers ya Algeria, utakaopigwa kesho, kwenye Uwanja wa Kasarani, kuanzia saa moja jioni, atajumuisha wachezaji kadhaa waliomvutia kwenye kikosi chake.

"Kuhusu Gor Mahia, niweke wazi kuwa nimeshawasiliana na Dylan Kerr, nilikuwa pale Kasarani siku ya Jumapili, nimevutiwa na baadhi ya wachezaji wa Gor, wakimalizana na USM Algiers, tutakuwa nao," alisema Migne.

Aidha, Kocha Hugo, aliyepewa mikoba ya kuinoa Stars, akimrithi Paul Put, alisema katika kikosi chake atawajumuisha maproo wanaosakata kabumbu nje ya nchi huku akisisitiza nahodha atasalia kuwa, Victor Mugubi Wanyama, anayekipiga na Tottenham Hotspurs ya England.