In Summary
  • Kocha wa zamani wa Manchester United, Jose Mourinho amesema kamwe hawezi kurejea Ureno kufundisha soka licha ya kuhusishwa na mpango wa kujiunga na klabu yake ya zamani Benfica.

Lisbon, Ureno. Jose Mourinho amesema hana mpango wa kuinoa Benfica inayoshiriki mashindano ya Ligi Kuu Ureno.

Kauli ya Mourinho imekuja muda mfupi baada ya kocha huyo wa zamani wa Manchester United kuhusishwa na mpango wa kuifundisha Benfica.

Benfica haina kocha baada ya Rui Vitoria kuondoka na klabu hiyo. Mourinho alifukuzwa Man United Desemba 18, mwaka jana.

“Sijapokea ofa yao, na kama itakuja lakini nataka Rais wa Banfica wafahamu uamuzi wangu mapema,” alisema kocha huyo aliyewahi kuzinoa klabu kubwa Ulaya.

Mourinho aliyewahi kuzinoa FC Porto, Inter Milan, Chelsea, Real Madrid na Man United, alisema hawezi kurejea nyumbani kwao Ureno kufundisha soka.

Pia Mourinho aligoma kuzungumzia sakata lake na Man United akidai siyo muda mwafaka na tayari kwasasa ni kocha huru.

Kocha huyo alianza kufundisha soka mwaka 2000 katika klabu ya Benfica kabla ya kutua FC Porto.

“Nimejifunza kitu, siyo jambo jema kuzungumzia mambo yaliyopita, huwezi kusafisha mikono michafu mbele ya jamii. Ukurasa umefungwa,” alisema Mourinho.