In Summary
  • Kocha wa AC Milan, Gennaro Gattuso amekunwa na kiwango na uwezo wa kufunga mabao muhimu alionao kiungo mpya wa timu hiyo Gonzalo Higuain, aliyetua kwa mkopo akitokea kwa bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Italia, Juventus iliyomuza kwa mkopo ili kupata fedha za kuongezea kumnunua Cristiano Ronaldo kutoka Real Madrid.

Milan, Italia. Kocha wa timu ya AC Milan, Gennaro Gattuso, ni kama anaishukuru Juventus iliyofanya uamuzi tata wa kuwazia kwa mkopo kiungo mshambuliaji Gonzalo Higuain.

Juventus iliamua kumuuza kwa nguvu Higuain ili kumpisha mshambuliaji wao mpya Cristiano Ronaldo, aliyenunuliwa kwa Euro 100 milioni kutoka Real Madrid Julai mwaka huu.

Alisema Higuain raia wa Argentina aliumia sana kutokana na namna alivyouzwa licha ya kuwa alikuwa mmoja wa wachezaji walioifungia Juve mabao muhimu akifunga mabao 55 katika mechi 105 alizocheza.

“Kwa namna moja ama nyingine ujio wa Higuain umekuwa na neema kwetu kwani tayari amefubnga mabao sita katika mechi saba alizocheza, tutajitahidi awe na furaha hapa AC Milan, ili aendelee kufunga mabao,” alisema Gattuso.

Naye mshambuliaji wa zamani wa Juventus, Alessandro del Piero, alielezea kutoridhishwa kwake na uamuzi uliofanywa na klabu hiyo wa kumuuza Higuain.

“Sikufurahishwa na namna klabu ilivyomtendea Higuain, hakukuwa na sababu ya kumuuza ili kumnunua Ronaldo, walipaswa kucheza pamoja alikuwa na mchango muhimu,” alisema Del Piero.

Alisema anaamini mchezaji huyo mwenye miaka 30 anaweza kuifanya Milan kuwa wapinzani wakuu wa Juventus katika ubingwa na kurejesha heshima iliyoanza kupotea San Siro.

Higuain mwenyewe alisema ili kuonyesha kuwa alichofanyiwa hakijamfurahisha atajitahidi kuelekeza nguvu zake zote katika klabu yake mpya ili kuipa mafanikio.