In Summary
  • Mshambuliaji nyota wa zamani wa Chelsea na timu ya Taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba 40, ambaye anamiliki timu ya soka ya Phoenix Rising jana alifunga bao katika ushindi 2-1 na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Western Conference michuano muhimu katika soka la Marekani.

Los Aneles, Marekani. Mshambuliaji mahiri wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba ambaye ni mmiliki wa klabu ya Phoenix Rising, jana alifunga bao lililoiwezesha timu yake kutwaa ubingwa wa Kanda ya Magharibi ‘Western Conference’ katika michuano muhimu ya Marekani.

Nahodha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Ivory Coast, mwenye miaka 40, alifunga bao la pili katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Orange County katika mechi ya fainali ya kanda hiyo.

Drogba ameandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza ambaye pia ni mmiliki wa timu kucheza na kufunga bao katika mechi muhimu na sasa Phoenix Rising itacheza na bingwa wa Kanda ya Mashariki timu ya Louisville City kumsaka bingwa wa USL Cup.

Mchezo huo wa kumsaka bingwa wa USL Cup utachezwa Alhamisi hii na wengi wanaamini kwa uwezo aliouonyesha Drogba anaweza kuendeleza miujiza yake katika soka kwa kuzamisha Louisville City.

Katika mechi ya jana Phoenix Rising ilianza kujipatia bao la kuongoza katika dakika ya pili kabla ya Drogba kutumia uzoefu wake kufunga bao la pili dakika ya 73 baada ya kuuwahi mpira alioupiga na kuzuiwa na beki.

Vijana wa Orange County, wakijitahidi kupambana na wakajipatia bao la kwanza lililofungwa na Chris Cortez aliyemalizia kazi nzuri iliyofanywa na Kevon Lambert dakika ya 81.

Haijajulikana kama huu utakuwa msimu wa mwisho kwa Drogba kuitumikia timu hiyo au la kwani mkataba wake wa sasa unamalizika mwishoni mwa mwezi huu.

Drogba aliyetwaa kila taji akiwa Chelsea alijiunga na Phoenix Rising, Aprili 2017 na baada ya klabu hiyo kuwekwa sokoni alijitosa kununua hisa kutoka kwa Berke Bakay na kuwa mmiliki wa klabu huku ni mchezaji.

Mshambuliaji huyo aliyeifungia Chelsea, mabao 164 katika mechi 381 alisema atahakikisha anafanya kila liwezekanalo kuipandisha Phoenix Rising iliyo Daraja la pili katika Ligi Kuu Marekani.

Drogba ambaye amecheza soka pia katika klabu za Le Mans, Guingamp, Marseille, Shanghai Shenhua, Galatasaray na Montreal Impac.

Akizungumza baada ya mchezo huo Drogba alisema ndoto zake ni kuona timu hiyo inapanda daraja na kucheza Ligi Kuu ya Marekani.

Alibainisha kuwa atafanikisha hilo kwani kuna mambo kadhaa ya kiutawala anayojifunza kutoka kwa mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich, ambaye awefanikiwa kwa kiasi kikubwa.