In Summary
  • England ilianza kujipatia goli kupitia kwa Kieran Trippier dakika ya tano baada ya kupiga mkwaju wa adhabu ndogo uliokwenda moja kwa moja nyavuni.

Croatia wameingia fainali za kombe la dunia kwa mara ya kwanza katika historia, baada ya kuichapa England 2-1 katika mchezo ambao ulichezwa kwa dakika 120.

England ilianza kujipatia goli kupitia kwa Kieran Trippier dakika ya tano baada ya kupiga mkwaju wa adhabu ndogo uliokwenda moja kwa moja nyavuni.

Kipindi cha kwanza kiliisha kwa England kwenda mapumzikoni ikiwa kifua mbele.

 

Kipindi cha pili Croatia ilitumia muda mwingi kumiliki mpira na kufanikiwa kusawazisha kupitia kwa Ivan Perisic aliyeonyesha kandanda safi na kuwa nyota wa mchezo.

Goli hilo liliupeleka mchezo huo kwenda dakika 30 za nyongeza huku kila timu ikicheza kwa tahadhari ya hali ya juu.

 

Hatimaye mshambuliaji wa Juventus ya Italia Mario Mandzukic akaandika goli la pili na la ushindi kwa Croatia na hivyo kutinga fainali itakayochezwa dhidi ya Ufaransa katika uwanja wa Luzhniki mjini Moscow Julai 15.

Croatia ni taifa la watu milioni nne hivi na ni moja ya mataifa yenye idadi ndogo sana ya watu kuwahi kufika fainali Kombe la Dunia.

England itacheza na Ubelgiji katika mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu Julai 14.