In Summary

Chirwa alikuwa mfungaji bora wa Yanga msimu uliopita akiwa na mabao 13, anasajiliwa na Azam kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba nchini Misri alikokuwa anachezea timu ya Nogoom El Mostakbal.

Klabu ya Azam FC imemsajili nyota wa zamani wa Yanga, Obrey Chirwa.
Chirwa ambaye alikuwa mfungaji bora wa Yanga msimu uliopita akiwa na mabao 13, anasajiliwa na Azam kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba nchini Misri alikokuwa anachezea timu ya Nogoom El Mostakbal.
Meneja wa Azam FC, Phillip Alando alisema kuwa klabu hiyo imemaliza na Chirwa huku akisubiri hatua zaidi za usajili baada ya dirisha kufunguliwa Novemba 15 mwaka huu.
"Tuko katika hatua za mwisho kabisa kumsajili Chirwa. Uhamisho wake umekamilika leo Alhamisi" alisema Alando.

Chirwa hivi karibuni alikuwa akihusishwa kutaka kusajiliwa na klabu yake ya zamani ya Yanga, hata hivyo kocha wa timu hiyo alifunguka na kuweka bayana suala hilo.

Mwinyi Zahera alisema sio jambo rahisi kuruhusu Chirwa kusajiliwa Yanga kutokana na nidhamu mbaya aliyoonyesha kwa klabu hiyo ya Jangwani.