In Summary
  • Hata hivyo kikosi hicho sasa kimeibuka kivingine baada ya kuwa na uhakika wa kuwatumia nyota wake wakali, Obrey Chirwa na Kelvin Yondani, ambao hawakuwa kikosini katika siku za karibuni.

Dar es Salaam. Hakuna ubishi kwamba Yanga imekuwa ikifanya vibaya katika mechi zake za karibuni, na hilo limezua wasiwasi iwapo timu hiyo ina uimara wa kufanya maajabu katika mechi ya leo Jumatano ya hatua ya makundi kuwania Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo kikosi hicho sasa kimeibuka kivingine baada ya kuwa na uhakika wa kuwatumia nyota wake wakali, Obrey Chirwa na Kelvin Yondani, ambao hawakuwa kikosini katika siku za karibuni.

Yondani na Chirwa wanarejea uwanjani baada ya kumaliza mgomo wa siku 25, waliouanzisha baada ya mchezo wa Yanga na ya Simba, Aprili 29 ambapo timu yao ilifungwa bao 1-0. Mgomo wao ulikuwa ni kushinikiza malipo ya baadhi ya stahiki zao wanazoidai klabu hiyo.

Kukosekana kwa wachezaji hao kulichangia matokeo mabaya ya Yanga kwenye michezo yake mitatu dhidi ya USM Alger, Prisons na Mtibwa Sugar ambapo walipoteza mechi zote.

Ilianza kwa kufungwa mabao 4-0 dhidi ya USM Alger kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho uliochezwa Mei 6 huko Algeria, ikaja kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu kwa kufungwa mabao 2-0 na Prisons Mei 10 kisha ikafungwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar, Mei 13.

Kukosekana kwa Yondani na Chirwa kwenye mchezo dhidi ya USM Alger, ndiko kuliiathiri zaidi Yanga kwani ilionekana kuwa na udhaifu mkubwa kwenye safu zake za ulinzi na ushambuliaji. Nafasi hizo zilionekana kupwaya na makosa ya maeneo hayo yaliishia kwa kupokea kichapo.

Matokeo ya 4-0 kwenye Kombe la Shirikisho yalifanya Yanga ishike mkia wa Kundi D, ambalo pia lina timu za USM, Gor Mahia na Rayon Sports.

Yanga inapaswa kuhakikisha inaibuka na ushindi kwenye mchezo wa leo, ili ifikishe pointi tatu ambazo zitafufua matumaini ya robo fainali huku pia wakingoja kuona matokeo ya Gor Mahia dhidi ya USM Algers jijini Nairobi leo.

Ikishindwa kupata ushindi, maana yake itabakia na mechi mbili tu za nyumbani, ambazo itatakiwa kuibuka na ushindi na kisha kulazimika kupigana kufa au kupona kwenye mechi zake mbili itakazobakiza ugenini dhidi ya Rayon Sports na Gor Mahia jambo ambalo litawaweka wawakilishi hao wa Tanzania kwenye wakati mgumu mbele ya safari.

Kwa kutambua umuhimu wa mchezo huo wa nyumbani, Yanga inaonekana imeivalia njuga Rayon Sports kuelekea mchezo wa leo, kwa kufanya maandalizi makubwa yakiwemo kuhakikisha Yondani na Chirwa wanacheza mechi hiyo, wakiamini watakuwa chachu ya kuvuna pointi tatu.

Kurudi uwanjani kwa Yondani leo, kunaiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kuwa imara kwenye safu yake ya ulinzi, kutokana na uwezo wa mchezaji huyo katika kuituliza timu pindi inaposhambuliwa pia umakini na hesabu nzuri pale anapokabiliana na washambuliaji wa timu pinzani sambamba na uwezo wake wa kupora mipira pindi timu yake inapopelekewa mashambulizi.

Kurejea kwa Chirwa ni muhimu katika kuimarisha safu ya ushambuliaji ya Yanga, kutokana na uwezo wa mchezaji huyo katika kufunga na kutengeneza nafasi za mabao pamoja na kuwachosha mabeki wa timu pinzani, akibebwa na kasi, nguvu na matumizi ya akili uwanjani.

Hata hivyo wakati Yondani na Chirwa wakitarajiwa kuiongoza Yanga leo, kiungo tegemezi Papy Tshishimbi ataendelea kukosekana kutokana na majeruhi, sambamba na Ibrahim Ajibu, ambaye ana ruhusa maalum wakiungana na Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambao ni majeruhi wa muda mrefu.

Kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila alithibitisha kurejea wa Yondani na Chirwa pamoja na kukosekana kwa Tshishimbi na Ajibu huku akisifu maandalizi yao kuelekea mchezo huo.

“Yondani na Chirwa wapo kikosini na wamefanya mazoezi ya pamoja na timu. Tshishimbi alirejea kwao baada ya kupata majeraha, kuhusu Ajibu nilisikia kwamba ana matatizo ya kifamilia hivyo meneja ndio ataweza kulizungumzia vizuri jambo hilo.”

Kuhusu ratiba alisema; “Ratiba haikuwa rafiki kwetu kwa sababu baada ya kutoka Algeria ilitubidi tusafiri tukacheze na Prison, tukaamua tuweke kikosi kingine hapa ili kijiandae na mechi, wapinzani wetu ni wazuri ndio maana wapo katika hatua ya makundi hivyo tunaamini mchezo utakuwa mzuri na tunahitaji ushindi.”

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliwaomba mashabiki wa timu hiyo na wadau wa soka nchini, kuweka kando changamoto zote ambazo klabu hiyo imezipitia katika siku za hivi karibuni na kuisapoti timu ili iweze kuvuna pointi tatu nyumbani.

“Kikubwa mashabiki watuunge mkono na wasikate tamaa, tunataka tupate ushindi katika mechi ya nyumbani ili iwe mtaji kwetu,” alisema.