In Summary
  • Chama alikosekana katika mechi hizo kwa kukosa hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) ambayo ilichelewa kufika nchini, lakini sasa uongozi wa Simba umeshamaliza kadhia hiyo.

Mtwara. Kiungo fundi wa Simba Mzambia Cletus Chama, kesho anatarajiwa kuichezea timu yake mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kukosekana katika mechi mbili za mwanzo dhidi ya Tanzania Prison na Mbeya City zote za Mbeya.

Chama alikosekana katika mechi hizo kwa kukosa hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) ambayo ilichelewa kufika nchini, lakini sasa uongozi wa Simba umeshamaliza kadhia hiyo.

Katika mechi ya kesho Chama anapewa nafasi kubwa ya kuanza katika kikosi cha kwanza kutokana na umahiri wake alionesha katika mechi tatu za kirafiki ambazo Simba walicheza kabla ya ligi kuanza.

Chama alionesha soka safi la kiwango cha juu na kuwapa mashabiki wa Simba kitu cha kutambia kwani aliupiga mpira mwingi katika ‘Simba Day’ dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana na mbili za kirafiki dhidi ya Namungo ya Lindi na Arusha United.

Kukosekana kwake katika mechi tatu za kimashindano ambazo zilikiwa dhidi ya Mtibwa Sugar katika mechi ya Ngao ya Jamii na mbili za ligi kulifanya mashabiki kumuuliza na kuhataji uwepo wake.

Kiungo Hassan Dilunga aliyesajiliwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar aliyechukua nafasi yake, ameumia goti na hatakuwepo katika mchezo wa kesho ndio maana Chama ana nafasi kubwa ya kucheza.

Dilunga alicheza vema akifunga bao murua katika mechi ya Ngao ya Jamii na kutoa pasi ya bao jingine lililofungwa na Meddie Kagere na Simba kushinda 2-1.

Mratibu wa Simba, Abbas Selemani alisema Chama aliwasili Mtwara akitokea moja kwa moja nchini Gambia ambako aliiwakilisha Zambia katika mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika zitakazopigwa mwakani nchini Cameroon.