In Summary
  • Msimu huu ambao utamalizika kesho kwa mchezo wa fainali kati ya Azam dhidi ya Simba, umeshirikisha jumla ya timu 12 ambazo ziligawanywa kwenye makundi matatu.

Dar es Salaam. Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa),  limepanga kuongeza idadi ya timu tatu zitazoshiriki mashindano ya Kombe la Kagame msimu ujao.

Msimu huu ambao utamalizika kesho kwa mchezo wa fainali kati ya Azam dhidi ya Simba, umeshirikisha jumla ya timu 12 ambazo ziligawanywa kwenye makundi matatu.

Akizungumzia kuongezeka kwa idadi ya timu hizo  kwa msimu ujao, katibu wa baraza hilo kongwe Afrika, Nicolaus Musonye alisema wanaweza kuongeza kutokana na maombi ya mataifa matatu ambayo wameyapokea.

"Mashindano yameenda vizuri, tumejitahidi kwa uwezo wetu kutengeneza mazingira bora kwa kila timu iliyoshiriki kuanzia kwenye usafiri, malazi na hata chakula.

"Maombi ambayo tumeyapokea ni kutoka kwenye mataifa ya DR Congo, Malawi na Zambia kwa maana hiyo kikao chetu cha hivi karibuni kitatoa uamuzi ya kukubali maombi hayo, " alisema Musonye.

Kuhusu idadi ya timu ambazo wataziongeza kwenye mashindano hayo ya msimu ujao, Musonye alisema zitakuwa tatu ili kuwa na makundi manne.

Kama kikao kijacho cha Cecafa kitapitisha kushiriki kwa timu kutoka katika mataifa hayo, huenda Simba, Yanga au Azam wakaanza kukutana na miamba ya nchi hizo kwenye kombe hilo la Kagame.

Pia Musonye alizungumzia kuhusu juhudi zao za kutaka mashindao hayo kuwa kwenye kalenda ya FIFA zimefikia pazuri na muda wowote michuano hiyo itatambuliwa rasmi na shirikisho hilo la soka Duniani.

Musonye alidai kwa namna ambavyo wameyaendesha mashindano hayo na kuzingatia uongozi wao mpya wa Cecafa kuna kila dalili za michuano hiyo kuwa bora zaidi Afrika kwa kulinganisha na kanda nyingine.

"Kupitia Kagame timu zetu zitapata ushindani wa kutosha utakao wajenga kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na Shirikisho," alisema Musonye