In Summary

Unaweza kujiuliza, kuna maswali kuhusu uwezo wao? Unaweza kupata majibu mchanganyiko, lakini mabao yao ndiyo yanayoibeba Simba.

Dar es Salaam. Pacha inayoundwa na washambuliaji John Bocco na Emmanuel Okwi imeendelea kuwa tishio kwa mabeki wa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Unaweza kujiuliza, kuna maswali kuhusu uwezo wao? Unaweza kupata majibu mchanganyiko, lakini mabao yao ndiyo yanayoibeba Simba.

Bocco alitia mpira kimiani dakika ya 35 kwa kichwa cha kuchupa na Okwi alifunga dakika ya 78 kwa mkwaju wa penalti.

Mabao hayo, yameiweka Simba katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Iko hivi, Simba inachotakiwa ni kushinda mechi tano kutawazwa ubingwa kwani itafikisha pointi 73 ambazo haziwezi kufikiwa na watani wao wa jadi Yanga ambao endapo watashinda michezo minane itafikisha pointi 71.

Mchezo wa jana ulichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Simba kufikisha pointi 58 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 47.

Simba imecheza mechi 24 na Yanga ambayo kesho itacheza mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Welaytta Dicha, imeteremka uwanjani mara 22.

Nahodha huyo wa Simba, alifunga bao hilo akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Erasto Nyoni kutoka upande wa kushoto na kugonga mwamba kabla ya kurudi uwanjani na kumkuta mfungaji.

Simba ilipata bao la pili dakika 78 kwa bao la mkwaju wa penalti lililofungwa na Okwi baada ya Bocco kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari na beki Jumanne Elfadhil.

Hata hivyo, adhabu ya penalti ililalamikiwa kwa dakika kadhaa baada ya wachezaji wa Prisons kumzonga mwamuzi Shomari Lawi wa Kigoma wakidai haikuwa halali.

Pia Lawi alimtoa Elfadhil kwa kadi nyekundu kwa kosa hilo.

Muungano wa Bocco na Okwi, umetengeneza pacha maridadi iliyoandika rekodi ya kufunga jumla ya mabao 33 katika mechi 24 za Ligi Kuu.

Okwi, mchezaji wa kimataifa wa Uganda anaongoza kwa kufikisha mabao 19 na Bocco amepachika 14.

Kufungwa kwa bao hilo kuliamsha ‘hasira’ ya Prisons ambayo ilisimama imara kumudu vyema kasi ya Simba isiongeze bao jingine.

Sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza Prisons ilijilinda huku ikifanya mashambulizi ya kushtukiza mbinu ambayo ilionekana kukaribia kuzaa matunda ingawa ilitibuliwa na mabeki wa Simba.

Licha ya kufungwa, Prisons ilifanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Simba, lakini hayakuzaa matunda.

Bocco alisema Prisons ni timu nzuri na ilijiandaa kucheza kwa kujilinda, lakini Simba ilivunja mtego huo na kufanya mashambulizi langoni mwao.

Pia alisema malengo yake ni kufunga mabao ili kuipa Simba ubingwa, lakini siyo kuleta ushindani wa kuwania tuzo ya mfungaji bora msimu huu.

Nayo Kagera Sugar iliichapa Mtibwa mabao 2-1, Ruvu Shooting iliilaza Ndanda 3-1 mkoani Mtwara.