In Summary
  • Stars wataanza kwa kucheza ugenini dhidi ya Algeria Machi 22, 2018 na siku tano baadaye watareja nchini kuwakabili DR Congo Machi 27, 2018 Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

 Kocha wa zamani wa Kenya, Mbelgiji Adel Amrouche wakati wowote kuanzia sasa atachukua mikopa ya Salum Mayanga kuinoa Taifa Stars

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu wa karibu na kocha huyo wamedai kocha huyo atasaini mkataba wa miaka miwili wa kuinoa Taifa Stars.

Chanzo hicho kimedau kocha huyo Mbelgiji mwenye asili ya Algeria tayari amefikiana makubaliano na vigogo wa  TFF, ila muda atakaoanza kazi haujafahamika.

Ujio wa kocha huyo ndiyo uliochangia kwa viongozi wa TFF kuomba mechi za kirafiki dhidi ya Algeria na DR Congo mwezi huu ili kuwaona wachezaji atakaohudumia katika mbio za kufuzu AFCON mwakani.

Mkataba wa Mayanga ulimalizika mwezi uliopita na TFF imekuwa kimya kuhusu kumuogezea mkataba mpya.

Hata jana wakati wa kutangaza kikosi cha Taifa Stars kitakachocheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Algeria na DR Congo, Mayanga hakuwepo katika mkutano na wanahabari ila msaidizi wake Hemed Morocco ndiye aliyekuwepo.

Kocha Amrouche si mgeni Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati mbali ya kuifundisha Harambee Stars kati ya 2013-14 baada ya kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Burundi kati 2007-12. Pia, ameifundisha klabu ya DC Motema Pembe ya DR Congo kati ya 2005-06.

Amrouche aliondoka Kenya 2014 akiwa na rekodi ya kuipa nchi hiyo ubingwa wa kwanza wa Kombe la Chalenji 2013 baada ya kukosa kwa miaka 11,  akichapa Tanzania 1-0 kwenye nusu fainali ya Kombe la Chalenji 2013 na kunyakuwa ubingwa huo kwa kuwanyuka Sudan 2-0.

Pia, aliiongoza Harambee Stars kucheza mechi 16 na kupoteza mechi tatu tu ikiwa ni rekodi ya kwanza tangu 1983.

Taifa Stars inategemea kuingia kambini Machi 18 na kuondoka Machi 19 kuelekea nchini Algeria kwa mchezo huo wa kirafiki ukaochezwa Machi 22.

Algeria kwa sasa ipo nafasi 60 katika orodha ya viwango vya ubora wa Fifa wakati Tanzania ikiwa nafasi ya 146 iwapo Tanzania itashinda itapanda zaidi katika orodha hiyo ya Fifa.

Baada ya mechi hiyo siku Machi 27, Stars itarejea nchini kujiandaa na mechi nyingine ngumu zaidi dhidi ya DR Congo iliyo nafasi ya 39, katika orodha ya ubora wa Fifa.

Taifa Stars na DR Congo wamekutana mara tano tangu 1995, mara mbili katika mechi za mashindano na mara tatu katika michezo ya kirafiki.

Tanzania imeshinda mechi mara mbili, sare moja na kufungwa mechi mbili mara ya mwisho zilipokutana Februari 23, 2012 timu hizo zilitoka suluhu.

Kikosi hicho kitaundwa na makipa, Aishi Manula (Simba), Ramadhani Kabwili (Yanga), Abdulraham Mohammed (JKU).

Mabeki ni Shomari Kapombe (Simba),Hassan Kessy (Yanga),Gadiel Michael (Yanga),Kelvin Yondani (Yanga), Abdi Banda (Baroka), Erasto Nyoni (Simba).

Viungo ni Hamisi Abdallah (Sony Sugar), Mudathir Yahya (Singida United), Said Ndemla (Simba), Faisal Salum (JKU), Abdulazizi Makame (Taifa Jang'ombe), Farid Mussa (CD Tenerife), Ibrahim Ajib (Yanga), Shiza Kichuya (Simba) Mohammed Issa (Mtibwa Sugar) na Thomas Ulimwengu.

Washambuliaji ni Mbwana Samatta (KRC Genk), Saimon Msuva (Difaa El Jadida), John Bocco (Simba), Zayd Yahya (Azam).