In Summary

Wafaransa roho kwatu, fainali kupigwa Jumapili

Moscow, Russia. Ufaransa imefuzu fainali ya Kombe la Dunia, baada ya kuifunga Ubelgiji bao 1-0, katika mchezo mkali uliochezwa kwenye Uwanja wa St Petersburg nchini Russia.

Ufaransa imepania kurudia rekodi ya mwaka 1998 ilipotwaa ubingwa wa Kombe la Dunia katika fainali zilizochezwa nchini humo huku kocha wa sasa wa timu hiyo, Didier Deschamps akiwa nahodha.

Bao pekee lililofungwa na beki wa kati wa Ufaransa anayecheza klabu ya Barcelona Samuel Umtiti, liliipeleka Ufaransa fainali. Timu hiyo inasubiri mshindi wa mchezo wa kesho baina ya England na Croatia kucheza fainali Jumapili wiki hii mjini Moscow.

Umtiti alifunga bao hilo dakika ya 51 akifunga kwa mpira wa kichwa akiunganisha kona, baada ya kumzidi maarifa mchezaji wa kiungo wa Ubelgiji, Marouane Fellani aliyeshindwa kumdhibiti.

Dakika 45 za mwanzo Ubelgiji ilicheza soka maridadi huku nahodha wake Edin Hazard anayecheza klabu ya Chelsea akicheza kwa kiwango bora ingawa mashuti yake mengi yalitua mikononi mwa kipa mkongwe Hugo Lloris.

Licha ya Ubelgiji kutawala sehemu kubwa ya mchezo, lakini ilishindwa kupenya ukuta uliokuwa chini ya beki wa Real Madrid Raphael Verane na Umtiti.

Ufaransa ilifuzu nusu fainali baada ya kuilaza Uruguay mabao 2-0 wakati Ubelgiji ilipenya kwa ushindi wa mabao 2-1 ilipovaana na Brazil.

Katika mechi 74 ilizokutanisha timu hizo, Ubelgiji imeshinda mara 30, Ufaransa imeshinda mechi 25 na miamba hiyo imetoka sare katika michezo 19.