In Summary
  • Kocha huyo wa Ufaransa, alisema leo ni kufa au kupona kwa nyota wake, lakini lazima ushindi dhidi ya majirani zao upatikane.

Moscow, Russia. Didier Deschamps  amewataka wachezaji wake kufia uwanjani katika mchezo wa leo wa nusu fainali dhidi ya Ubelgiji.

Kocha huyo wa Ufaransa, alisema leo ni kufa au kupona kwa nyota wake, lakini lazima ushindi dhidi ya majirani zao upatikane.

Ufaransa na Ubelgiji zinajitupa uwanjani kuwania pointi tatu muhimu ili kukata tiketi ya kufuzu fainali ya Kombe la Dunia mwaka huu.

Nahodha huyo wa zamani aliyeipa Ufaransa ubingwa wa dunia mwaka 1998, alitoa kauli hiyo wakati wa mazoezi ya kikosi hicho leo kabla ya kuivaa Ubelgiji saa tatu usiku.

“Leo tuna nafasi ya kucheza fainali ya Kombe la Dunia. Tunapaswa kufanya kila njia kupata ushindi,” alisema nyota huyo wa zamani wa Chelsea.

Alisema hakuna sababu ya kushindwa kupata ushindi katika mchezo huo kwa kuwa ana kikosi bora cha kushindana.

Ufaransa leo ilifanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuteremka uwanjani kumenyana na wapinzani wao ambao wananolewa na kocha Roberto Martinez.