Moscow, Russia. Nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa na klabu ya Arsenal, Thiery Henry ambaye kwa sasa anaitumikia timu ya taifa ya Ubelgiji, kama msaidizi wa Kocha Roberto Martinez, amekuwa gumzo kuelekea mchezo kati ya timu hizo mbili.

Ubelgiji na Ufaransa zitajitosa dimbani usiku wa leo, kutafuta nafasi ya kutinga fainali ya michuano ya Kombe la Dunia, inayoelekea ukingoni. Mchezo huo wa kukata na shoka ya nusu fainali ya kwanza, itapigwa kwenye dimba la St. Petersburg, yenye uwezo wa kuchukua mashabiki 67,000.

Hata hivyo, wakati mafahali hao wakijiandaa kutoana jasho, macho na masikio yameelekezwa kwa Thiery Henry. Kila mtu anataka kuona atafanya nini katika mchezo wa leo. Je, atacheka au atanuna, atashangalia au atalia. Swali kubwa likiwa ni je, Henry ataheshimu kazi au Uzalendo bao litakapofungwa?

Itakumbukwa kwamba, Henry aliiongoza Les Blues kutwaa Kombe la Dunia 1998, katika ardhi yao ya nyumbani wakiitandika Brazil 3-0, kabla ya kuisaidia kutwaa ubingwa wa Kombe la Euro, mwaka 2000.

Miaka 20 baada ya usiku wa Historia wa Paris, Straika huyu wa zamani wa Arsenal, atakuwa katika benchi la ufundi la Red Devils akisuka mipango ya kuliangamiza taifa lake. Mechi hii, itamkutanisha na nahodha wake wa zamani, Kocha mkuu wa Les Blues, Didier Deschamps.

Kama hiyo haitoshi, Henry leo atakutana na nyota mmoja aliowahi kucheza naye pamoja kuitetea bendera taifa la ufaransa, Kipa Hugo Lloris. Kila mtu anamuangalia yeye, Dunia nzima inamuangazia Thiery Henry, Je, atachagua uzalendo au atalinda kazi yake? Patamu hapo!

Wakati ulimwengu ukisubiri kutegua cha nani mkali kati ya Ufaransa na Ubelgiji. wakati ulimwengu ukiwa na shauku kubwa ya kuutizama uso wa Henry Ufaransa itakapotobolewa au kufunga bao, Kocha Didier Deschamps na nahodha wa Les Blues, Hugo Lloris wanaamini Henry atakuwa muungwana.