In Summary
  • Enrique Kocha wa zamani wa Barcelona na AC Roma, amesaini mkataba wa miaka miwili kuinoa timu ya Taifa ya Hispania kuchukua nafasi ya Kocha wa muda Fernando Hierro, aliyejiuzulu Jumapili iliyopita baada ya kushindwa kuivusha Hispania katika hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia 2018.

Madrid, Hispania. Kocha mteule wa Hispania, Luis Enrique, ameahidi kuirejeshea nchi hiyo heshima yake katika medani ya soka la kimataifa.
Enrique Kocha wa zamani wa Barcelona na AC Roma, amesaini mkataba wa miaka miwili kuinoa timu ya Taifa ya Hispania kuchukua nafasi ya Kocha wa muda Fernando Hierro, aliyejiuzulu Jumapili iliyopita baada ya kushindwa kuivusha Hispania katika hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia 2018.
Hierro aliteuliwa muda mfupi kabla ya kuanza kwa fainali hizo za 21 za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Russia akichukua nafasi ya Julen Lopetegui, aliyefukuzwa siku tatu kabla ya Hispania kucheza na Ureno.
Enrique aliyeinoa Barcelona kwa nyakati tofauti mwaka 2014 na 2017, ametia saini mkataba huo huku akimuahidi Rais wa Shirikisho la soka Hispania (RFEF), Luis Rubiales, kuwa atafanya kila awezalo kurudisha heshima ya Taifa hilo.
Alisema nia yake ni kuona Hispania mabingwa wa Dunia mwaka 2010 wanarejea katika zama za kutamba kisoka barani Ulaya na duniani kwa ujumla, jambo ambalo anaamini litafanikiwa iwapo atapewa ushirikiano wa kutosha na wadau wote.
Enrique, aliyepata kuzichezea timu zote kubwa Hispania za Real Madrid na Barcelona, akitwaa mataji yote makubwa mtihani wake wa kazi utaanzia ugenini dhidi ya England kwenye dimba la Wembley, Septemba 8 mwaka huu katika mchezo wa kuwania tiketi ya michuano ya Euro 2020.
Mbali ya Enrique RFEF pia imemtangaza kipa wa zamani wa Hispania, Francisco Molina kuwa Mkurugenzi wa Ufundi na kwamba wasaidizi wa Kocha huyo watatangazwa baadaye.