In Summary
  • Simbu anapigia hesabu zaidi ya Sh200 milioni kwenye mbio hizo zilizopangwa kufanyika Novemba 4, Marekani.

Bingwa wa mbio za New York City Marathoni, Geoffrey Kamworor anakabiliwa na kibarua kigumu mbele ya nyota wa riadha Tanzania, Alphonce Simbu.

Simbu anapigia hesabu zaidi ya Sh200 milioni kwenye mbio hizo zilizopangwa kufanyika Novemba 4, Marekani.

Mwanariadha huyo anayejifua kwenye eneo la misitu na milima ya Ilboru, Arusha ana nafasi kubwa ya kuvuna dola 100,000 (zaidi ya Sh200 milioni).

Fedha hizo ambazo ni zawadi kwa mshindi, anaweza kuzipata Simbu endapo atampiku mpinzani wake mkubwa Kamworor raia wa Kenya ambaye ni bingwa mtetezi wa mbio hizo.

Katika mbio za mwaka jana, Kamworor alivuna fedha hizo baada ya kutumia saa 2:11.15 muda sawa na aliotumia Simbu kwenye Olimpiki ya Rio 2016 ambapo alimaliza kwenye nafasi ya tano.

Nyota huyo wa mbio ndefu nchini, ana rekodi nzuri ya saa 2:09:10 aliyoiweka kwenye mbio za London Marathoni na saa 2:09:51 katika mashindano ya Dunia mwaka jana nchini Uingereza alikoshinda medali ya fedha.

Mbali na Kamworor, Simbu pia atakuwa na kibarua cha kuchuana na nyota wengine wa mbio za New York City, Wilson Kipsang ambaye alimaliza kwenye nafasi ya pili mwaka jana akitumia saa 2:10:56 na Lelisa Desisa wa Ethiopia aliyemaliza wa tatu akitumia saa 2:11:32.

“Sina presha na ushindani, nimejipanga na bahati nzuri nimekuwa nikiboresha muda wangu katika mazoezi kila siku, hivyo sitafanya makosa, nahitaji medali, najiamini na ninaamini nina kiwango bora cha kubadili upepo wa matokeo kwenye mbio hizo,” alisema Simbu.

Habari njema ni kwamba hata akimaliza kwenye nafasi ya pili, Simbu atakuwa na uhakika wa kuweka mfukoni dola 60,000 wa tatu dola 40,000 na zawadi ya fedha inatolewa hadi kwenye 10 bora ambapo mshiriki anayeshika namba 10 ataondoka na dola 2,000.

Kocha wa timu ya Jeshi, Shabani Hiki alisema maandalizi anayofanya Simbu yanampa nafasi kubwa kutwaa ubingwa katika mbio hizo.