In Summary
  • Pia Simba ilikosa mkwaju wa penalti, baada ya mshambuliaji wake mpya, Adam Salamba kupiga shuti hafifu lililotua mikononi mwa kipa wa Asante Kotoko katika dakika ya 86.

Dar es Salaam. Kukosa umakini kwa mabeki na safu ya ushambuliaji, kumechangia Simba kukosa ushindi katika mchezo wa Sherehe za Simba Day.

Pia Simba ilikosa mkwaju wa penalti, baada ya mshambuliaji wake mpya, Adam Salamba kupiga shuti hafifu lililotua mikononi mwa kipa wa Asante Kotoko katika dakika ya 86.

Matokeo ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Asante Kotoko ni kama yametia doa sherehe za Simba Day jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Maelfu ya mashabiki wa Simba waliujaza uwanja huo kwa jezi za rangi nyekundu na nyeupe wakiamini Kotoko itashushiwa mvua ya mabao.

Mashabiki hao walikosa furaha waliyotarajia, baada ya Simba kukosa idadi kubwa ya mabao katika mchezo huo hasa kipindi cha kwanza.

Mchezo huo ulikuwa wa kwanza kwa Simba tangu iliporejea nchini kutoka Uturuki ilipoweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pia mchezo huo ulikuwa wa kwanza kwa kocha mpya Mbelgiji, Patrick Aussems kushindana na timu ngumu tangu alipochukua nafasi ya Pierre Lechantre.

Uzembe wa mabeki wa Simba kushindwa kuwadhibiti washambuliaji wa Asante Kotoko kulichangia kukaribisha mashambulizi ya kushitukiza langoni mwao.

Mshambuliaji wa Asante Kotoko aliyekuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Simba, Michael Yeboah aliifungia bao timu yake dakika ya 44 kwa mpira wa kichwa.

Yeboah alifunga bao hilo baada ya kuwahi mpira uliogonga mwamba wa juu baada ya kumzidi maarifa beki wa kati, Pascal Wawa.

Katika mchezo huo, Simba ilikosa nafasi nyingi za kufunga huku washambuliaji wake wakishindwa kumalizia pasi za mwisho.

Mshambuliaji tegemeo, Meddie Kagere alibanwa na mabeki wa Asante Kotoko kabla ya kutolewa na nafasi yake kujazwa na Salamba.

Licha ya kiungo mpya Mzambia Cletus Chama, aliyekuwa nyota wa mchezo huo, alifanya kazi nzuri ya kupenyeza mipira kwa akina Okwi na Salamba, lakini walishindwa kukwamisha mpira wavuni.

Okwi aliisawazishia Simba bao dakika 76 kwa bao murua kwa pasi ya Shiza Kichuya.

Mashabiki lukuki

Mamia ya mashabiki wa Simba walianza kumiminika kwenye uwanja huo kuanza saa mbili asubuhi wakiwasili kwa mabasi mbalimbali na wengine kwa miguu.

Mashabiki hao walianza kuingia uwanjani kuanzia saa nne asubuhi na idadi kubwa walikwenda katika jukwaa la upande wa Magharibi huku bendi ya muziki wa dansi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ ikitumbuiza.

Kombe bandia

Katika hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya mashabiki waliingizwa mjini baada ya kutozwa fedha kwa kupiga picha na kombe bandia la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Mashabiki waliotaka kupiga picha na kombe walilipa Sh1,000 ambazo ziliishia mifukoni mwa wapigapicha ambao walikuwa na mashine ya kusafisha picha hizo.

Chid Benz apagawisha

Msanii wa muziki wa bongo fleva nchini, Rashid Makwiro ‘Chid Benz’ alinogesha tamasha hilo kwa maelfu ya mashabiki waliojitokeza uwanjani.

Kwa muda mrefu Chid Benz hakuwa akitamba katika muziki wa bongo fleva kutokana na matumizi ya dawa za kulevya, lakini jana alikonga nyoyo za maelfu ya mashabiki wa Simba.

Dalali arusha dongo

Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali, alipiga kijembe watani wao wa jadi Yanga akiwataka kuanzisha ‘Tamasha la Akilimali Day’ ili kuwafariji mashabiki wao.

“Simba iko vizuri tuna kikosi imara na wachezaji wametokea Uturuki na wenzetu wamekwenda kuweka kambi milimani huko Morogoro, lakini tamasha hili lina maana kubwa si vibaya wenzetu wakiiga na kuita Yanga Day au Akilimali Day,” alisema Dalali.

Kauli ya Lugola

Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola, aliyekuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo, alisema Serikali itaanza msako wa kusaka wauzaji wa jezi feki za klabu za soka nchini.

Lugola alisema muda mrefu klabu za soka zimekosa mapato kupitia jezi zao ambazo zimekuwa zikiuzwa mitaani na kuwanufaisha watu wengine nje ya klabu husika.

Kocha Simba

Kocha Patrick Aussems alisema ameridhika na kiwango cha wachezaji wake licha ya kukosa ushindi katika mchezo huo. Alisema kambi ya Simba nchini Uturuki imekuwa na mafanikio, baada ya kucheza kwa kiwango bora dhidi ya timu ngumu.

“Tumecheza na timu ngumu, lakini najivunia mafunzo ya kambi yetu yamefanyiwa kazi ingawa nasikitika tumekosa penalti, ndio mchezo,” alisema Aussems.

Alisema anatarajia mchezo wa ufunguzi dhidi ya Mtibwa Sugar utakuwa mzuri kwa Simba kwa kuwa atakuwa amefanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika mchezo wa jana.

Kikosi Simba

Aishi Manula, Shomari Kapombe/Nicholaus Gyan, Asante Kwasi, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Cletus Chama, James Kotei/Hassani Dilunga, Meddie Kagere/Adam Salamba, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya.

Imeandaliwa na Thobias Sebastian, Charles Abel na Charity James.