In Summary
  • Mshambuliaji nyota na nahodha wa Brazil, Neymar, anayekipiga PSG ya Ufaransa ni kama amebadili msimamo baada ya kuzikataa ofa za Chelsea na Man City, sasa amefungua uwezekano wa kutua katika Ligi Kuu England.

Paris, Ufaransa. Mshambuliaji mahiri wa Brazil anayecheza Paris Saint-Germain ya Ufaransa, Neymar, amefungua milango ya kucheza soka katika Ligi Kuu England.

Neymar ambaye alipata kuikataa ofa ya kujiunga na Manchester City, hivi sasa amesema anadhani hivi anajisikia kwenda kucheza katika Ligi hiyo.

Mchezaji huyo alibainisha hayo wakati akijibu maswali aliyoulizwa kwenye mtandao wake wa kijamii na mashabiki pamoja na wachezaji mahiri miongoni mwa waliomuuliza maswali ni kiungo wa kimataifa wa Ufaransa, Benjamin Mendy, anayekipiga Man City.

Mendy alimuuliza "Neymar Jnr, tafadhali nijibu kwa Kifaransa, hivi unadhani kuna siku itatokea ukacheza katika moja ya timu za Ligi Kuu England?".

"Ni Ligi yenye ushindani mkubwa, moja ya Ligi zenye mvuto mkubwa duniani, hatuwezi kujua kwa sasa nini kitatokea kesho, lakini ninaamini kwa mchezaji yeyote bora kuna siku atacheza katika Ligi Kuu England,” alijibu Neymar.

Neymar aliendelea kusema anaamini mchezaji akicheza katika Ligi Kuu England, anafurahia na kufaidi uhondo wa ushindani uliopo katika Ligi hiyo ambayo ni bora na yenye msisimko.

Mbali ya hilo Neymar, pia amechukua ahadi ya kucheza katika timu ya Inter Miami CF iliyopo mjini Miami, Marekani inayomilikiwa na nahodha wa zamani wa Uingereza, David Beckham.

Kiungo huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid alimuuliza “Neymar pindi utakapomaliza kucheza soka barani Ulaya, utakuwa radhi kuja kucheza hapa Miami” alisema.

"David, hilo litakuwa, nakuahidi nitakuja Miami, kwenye jiji lako, kwenye timu yako,” Neymar.