In Summary
  • Biashara inatarajiwa kuikaribisha Kagera Sugar na Thiery amesema anaamini ushindi pekee ndio utawapa furaha wakazi wa Musoma na Mara.

Mwanza. Wakati timu ya Biashara United ikijiandaa kutumia uwanja wake wa nyumbani wa Karume kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu Tanzania Bara Jumamosi wiki hii, Kocha Hitimana Thiery amesema watahakikisha wanashinda mchezo huo.

Biashara inatarajiwa kuikaribisha Kagera Sugar na Thiery amesema anaamini ushindi pekee ndio utawapa furaha wakazi wa Musoma na Mara.

Alisema ingawa wapinzani wao wanajivunia uzoefu kwenye mashindano ya Ligi Kuu, ana matumaini timu yake itacheza soka maridadi ili kupata pointi katika uwanja wake wa nyumbani.

Kocha huyo alisema ametoa mafunzo ya kutosha kwa wachezaji na amewapa mbinu za kushinda mchezo huo.

“Tuna kila sababu ya kushinda mchezo dhidi ya Kagera Sugar kwa sababu kwa mara ya kwanza tutacheza nyumbani. Pia tunaufungua uwanja wetu kwa hiyo hatutaki kuwatia aibu mashabiki wetu, tumejiandaa vizuri tutahakikisha tunapata pointi tatu,”alisema Thiery.

Kocha huyo alisema wanataka kuthibitisha ubora wao kwa kupata ushindi katika mchezo huo kama ilivyokuwa dhidi ya Singida United. Biashara ina pointi tatu baada ya kucheza mechi tatu kwenye mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.