In Summary
  • Walitumia miaka mitano kusomea shahada ya uzamivu (PhD) katika Hisabati

Ilikuwa lazima umati wa watu katika hafla ile ulipuke mwa vifijo na nderemo.

Kusoma hesabu tena kwa ngazi ya shahada ya uzamivu (PhD), kunahitaji moyo thabiti.

Ni wanafunzi wachache vyuoni wanaoweza kusoma somo hilo kwa ngazi ya juu kama hii.

Kukitokea wanafunzi wanaohitimu ngazi hiyo, wanapaswa kupongezwa kwa kusoma kile ambacho mtazamo wa walio wengi ni kuwa hakisomeki.

Hata hivyo, pongezi zaidi ni kuona katika wachache hao kuna wanawake, ndio maana umati uliohudhuria sherehe ya mahafali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) hivi karibuni, uliripuka shangwe pale yalipotajwa majina ya wahitimu wawili wa kike waliotunukiwa shahada ya uzamifu katika Hisabati.

Hawa ni Dk Geomira Sanga na Dk Triphonia Ngailo waliochomoza kama wanawake wa mfano katika taaluma ambayo idadi ya wanawake haivutii hata kidogo.

Ndiyo maana siku ile ya mahafali walipongezwa na watu wengi, huku baadhi wakiwa hawaamini na kuwauliza namna walivyoweza kusoma hadi kutunukiwa shahada hiyo ya juu katika taaluma.

Kiuhalisia, wanawake wachache wamekuwa na ari ya kusoma hesabu kwa ngazi ya chuo kikuu. Takwimu za mradi wa hesabu unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Sweden (Sida), zinaonyesha kuanzia mwaka 2013 hadi 2018, wanawake waliohitimu shahada ya kwanza ya hesabu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, walikuwa 32, huku wanaume wakiwa 472.

Safari yao kielimu

Miaka mitano ya kutafuta shahada haikuwa kazi ndogo. Wamepitia changamoto mbalimbali zikiwamo za kifamilia, ugumu wa somo, ukosefu wa vifaa vya utafiti na nyinginezo.

Simulizi ya Dk Geomira

Dk Geomira ambaye sasa ni mwalimu wa hesabu katika chuo kikuu cha Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT), alianza safari ya kusaka shahada hiyo mwaka 2014, huku akichagua kufanya utafiti kuhusu hali ya kinga kwa waathirika wa Virusi vya Ukimwi (VVU) ambao pia wana Saratani ya Shingo Kizazi.

‘’Niliangalia kuhusu uwezekano wa kupanda au kushuka kwa kinga za mgonjwa huyu. Kina mama wengi sasa hivi wanapata saratani hii, nilijiuliza ukiwa na VVU unawezaje kujikinga na saratani ya shingo ya kizazi? ”anasema.

Shauku na mapenzi kwa hesabu Alianza tangu akiwa madaraja ya chini, huku akipata msukumo mkubwa kutoka kwa wazazi wake.

“Wazazi wangu walikuwa wakinipeleka katika makongamano mbalimbali ya hesabu na hata kunikutanisha na wasomi wenye shahada ya uzamifu ya hesabu, lengo tu nijifunze kutoka kwao...’’ anasema.

Dk Geomira ambaye katika mitihani ya elimu ya msingi na kidato cha nne hakuwahi kupata chini ya alama A anaongeza kusema:

“Nilikuwa navutiwa ninapoona watu mbalimbali wanatunukiwa PhD za hesabu nikwa najiuliza inawezekana vipi? Hivyo nilitamani siku moja watu washangae kuona kama kumbe hesabu ni nyepesi kama masomo mengine.’’

Shauku ya kujiendeleza zaidi katika somo hilo, anasema ilimjaa alipokuwa akisoma shahada ya uzamili katika masomo ya Kemia na Hisabati nchini Afrika ya Kusini. Alikutana na watu mbalimbali waliompa hamasa.

“Niliona wenzangu wanaweza, nikajiuliza kwa nini mimi nishindwe. Hapa ndipo mapambano yakaanza; niliomba ushirikiano wao walinisaidia na mpaka leo naamini ukitaka kuwa na mafanikio, lazima uwe karibu na watu waliofankikiwa,’’anasema.

Simulizi ya Dk Triphonia

Dk alianza safari yake 2014 akijikita katika utafiti kuhusu masuala ya hali ya hewa na akifanya uchunguzi wa hali ya mvua kwa miaka 50 ijayo.

“Nilikuwa nakusanya takwimu mbalimbali za hali ya mvua nchini na kuonyesha utabiri kwa kipindi cha miaka 50 hali itakuwaje,” anaeleza mtaalamu huyo wa hesabu anayesema hakuwahi kupata alama chini ya B ya Hisabati katika mitihani ya kidato cha nne na sita.

Dk Triphonia anayefanya kazi Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), anasema laiti angekuwa akiwasikiliza watu, angekuwa ameshakata tamaa siku nyingi.

“Nilianza kupenda hesabu tangu nikiwa mdogo na wazazi wangu walinijengea mazingira ya kuipenda hesabu. Siku zote walinisihi niache dhana potofu kuwa somo hilo halisomeki.”

Anasema hakuwahi kuogopa wala kulihofia somo hilo pamoja na dhana kwamba halieleweki, lakini alilipenda kama masomo mengine.

“Safari yangu iliendelea hivyo hadi nilipomaliza elimu ya msingi na kupata alama ya juu. Hata hivyo nilifanya vizuri kwa masomo mengine pia,” anaeleza.

Anasema katika jamii unapoonyesha jitihada katika kitu ambacho wengi wanakishindwa, unaweza kuonekana mtu anayependa sifa.

“Wakati mwingine hata wanafunzi wenzangu darasani walinitenga na kunichukia. Mimi nilishangaa sana badala wanitumie ili tuweze kusaidiana wao walikuwa wananichukia.”