In Summary

  • Kumekuwapo malalamiko mengi kuhusu wagombea kupita bila kupingwa, tena wote wakawa wa chama kimoja. Makala hii inaangazia taratibu za kisheria zinazomfanya mgombea atangazwe kupita bila kupingwa.

Wakati uchaguzi mdogo katika Jimbo la Liwale na kata 37 ukiwa katika hatua ya kampeni, msamiati wa mgombea kupita bila kupingwa katika kipindi hiki umekuwa ukiibua sintofahamu kwa wadau wengi wa uchaguzi.

Hali hii imetokana na kukosekana kwa ufahamu wa kisheria juu ya maana ya kupita bila kupingwa, mambo yasababisha na nini kinafanyika baada ya mgombea kupita bila kupingwa.

Kifungu cha 45 (2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, na kile cha 44 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, vinasema endapo mgombea aliyeteuliwa katika uchaguzi ni mmoja tu, mgombea huyo atahesabika amechaguliwa na Tume.

Tafsiri ya maneno “amechaguliwa na Tume” haina maana kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndiyo inamchagua mgombea huyo, bali Tume kwa kutimiza masharti ya vifungu hivyo, kupitia kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa ngazi husika, humtangaza mgombea huyo kwamba amepita bila kupingwa kupitia tangazo kwenye Gazeti la Serikali la kumtangaza mgombea huyo kuwa amechaguliwa kuwa mbunge au diwani.

Hata hivyo, hatua hii ya mgombea kupita bila kupingwa ni hitimisho tu la mchakato wa uteuzi wa wagombea kwa mujibu wa vifungu vya 37(1) (b) (5) na 46 (2) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na vifungu vya 13(3) na 41(3) vya Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa.

Baada ya Tume kutoa ratiba ya utoaji na urejeshaji fomu, Msimamizi wa Uchaguzi kwa niaba ya Tume kufanya uteuzi wa wagombea baada ya uchambuzi na kujiridhisha kuwa waombaji wamekidhi sifa, masharti na taratibu za uteuzi wa wagombea.

Sifa za mtu kuteuliwa kuwa mgombea ubunge au udiwani ni pamoja na kuwa mwanachama wa chama cha siasa ambacho kitampendekeza kugombea, awe na umri kuanzia miaka 21 na awe raia wa Tanzania.

Ajue kusoma na kuandika kwa Kiswahili au Kiingereza na kwa mgombea udiwani ni lazima awe mkazi wa halmashauri yenye kata anayogombea udiwani na awe na kipato halali kinachomwezesha kuishi.

Mbali na sifa hizo, mtu anayeomba kuteuliwa asiwe anatumikia kifungo cha zaidi ya miezi sita gerezani, asiwe uhamishoni au amezuiwa kisheria kuandikishwa kuwa mpigakura.

Mtu huyo hatakiwi kuwa na maslahi katika mkataba na halmashauri au kampuni yenye mkataba na halmashauri na hajajitangaza kwenye magazeti yanayopatikana kwenye halmashauri hiyo juu ya maslahi hayo.

Mtu anayeomba kuteuliwa kugombea ubunge au udiwani hatateuliwa iwapo amewahi kutiwa hatiani kwa kosa la kukwepa kulipa kodi kwa miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi husika.

Anatakiwa kuthibitisha kuwa yuko tayari kugombea na anazo sifa na kutoa tamko la kisheria la mgombea linalosainiwa na kuwekwa muhuri wa hakimu ili kuthibitisha yaliyomo.

Anayeomba kuteuliwa anatakiwa awe na wadhamini walioandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapigakura wasiopungua kumi (udiwani) au 25 (ubunge) walioandikishwa ndani ya jimbo analogombea.

Fomu ya uteuzi hutakiwa kuambatanishwa na picha nne za pasipoti zilizopigwa ndani ya miezi 3 kabla ya siku ya uteuzi, atatakiwa kulipa dhamana ya Sh 5,000 (Udiwani) na Sh 50,000 (Ubunge).

Fomu za uteuzi zinatakiwa kuwasilishwa kwenye Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi au msaidizi wake si chini ya saa kumi kamili jioni ya siku ya uteuzi na mgombea hutakiwa kujaza kwa usahihi Fomu Namba 10 ya kuheshimu na kutekeleza Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015.

Hata hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi hutoa nafasi kwa wagombea kupeleka fomu siku tatu kabla ya siku ya uteuzi ili zikaguliwe na kuona kama zimekidhi vigezo na masharti ya uteuzi na kisha hurudishiwa kwa mgombea ili kusubiri siku ya uteuzi.

Mgombea anatangazwa amepita bila kupingwa ikitokea wagombea wenzake wote wamekosa sifa za kuteuliwa na wameshindwa kukidhi masharti ya uteuzi ua kufuata taratibu za uteuzi kwa usahihi.

Au inawezekana wagombea wote wakapita kwenye uteuzi lakini wakawekewa pingamizi kwa mujibu wa kifungu cha 40 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi au kile cha 44 cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali ya Mitaa.

Vifungu hivyo vinatoa fursa kwa mgombea kuwekewa pingamizi iwapo maelezo yaliyotolewa na mgombea hayatoshelezi kumtambulisha, fomu yake ya uteuzi haikidhi au haikuwasilishwa kwa mujibu wa masharti.

Sababu nyingine ni iwapo kutokana na taarifa katika fomu ya uteuzi mgombea hana sifa za kuteuliwa kuwa, iwapo hakulipa dhamana na kama hajazingatia Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010.

Iwapo mgombea mmoja amewawekea pingamizi wagombea wenzake na akashinda basi iwapo atakuwa peke yake kati ya wagombea walioteuliwa, basi atatangazwa amepita bila kupingwa.

Lakini pia ikitokea wagombea walioteuliwa ni wawili na baadaye mmoja kujitoa kwenye uchaguzi, basi mgombea atakayebaki atatangazwa amepita bila kupingwa na hivyo kutangazwa kuwa amechaguliwa.

Mwandishi ni Afisa Habari, Tume ya Taifa ya Uchaguzi. [email protected] au 0717 148656