In Summary
  • Mara ya mwisho kwa mshindano hayo kufanyika ilikuwa 2015 nchini hapa ambapo Azam FC, ilitwaa ubingwa huo kwa kuifunga Gor Mahia ya Kenya kwenye fainali kwa mabao 2-0.

Baada ya miaka miwili bila ya mshindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘Kagame Cup’, hatimaye kombe hilo limerejea tena kwa Tanzania kuwa na mwenyeji wa mashindano hayo makubwa kwa ukanda huu.

Mara ya mwisho kwa mshindano hayo kufanyika ilikuwa 2015 nchini hapa ambapo Azam FC, ilitwaa ubingwa huo kwa kuifunga Gor Mahia ya Kenya kwenye fainali kwa mabao 2-0.

Kombe la Kagame lilianzishwa 1974 kwa lengo la kuinua soka la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mara ya kwanza kufanyika mashindano hayo, inatajwa ni 1967 lakini hayakuwa mashindano rasmi.

Wakati yakifanywa kuwa mashindano rasmi, 1974 Simba ambao ni mabingwa wa kihistoria kwenye mashindano hayo kwa kutwaa mara sita ndio iliyokuwa timu ya kwanza kuchukua kombe la Klabu Bingwa za Afrika Mashariki na Kati.

Udhamini wa rais wa Rwanda, Paul Kagame kuanzia mwaka 2002 ulifanya michuano hiyo mikongwe Afrika kupachikwa jina la kiongozi huyo ambaye ameiongoza nchi yake kwa zaidi ya miaka 10.

Hii ni awamu ya 13, Tanzania kupata uwenyeji wa kombe hilo ambao litaanza kutimua vumbi Juni 28 hadi Julai 13 kwenye Uwanja wa Taifa na Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Tanzania inawakilishwa na timu tatu, ikiwemo Simba ambayo imepata nafasi ya upendeleo kwa kuwa Tanzania ndiyo mwenyeji.

Rais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF,) Wallace Karia: “Tuna nafasi ya timu tatu kushiriki kwenye mashindano hayo, kwanza Azam anashiriki kwa bingwa mtetezi, Yanga ni bingwa wa ligi kwa msimu wa 2016/17”.

“Simba amepata nafasi ya ziada ya tatu kwa sababu tuna uwenyeji wa mashindano hayo.”

Makundi ya Kagame yamepangwa matatu na yatatoa timu mbili zitakazo fanya vizuri kwenye kila kundi huku kukiwa na nafasi kwa timu mbili za upendeleo ‘best loser’ ili kupata timu nane zitazocheza robo fainali.

Kundi A ni JKU (Zanzibar) , UGA (Uganda) , Azam (Tannzania) na Kator FC (Sudan Kusini).

Kundi B ni Rayon (Rwanda), Gor Mahia (Kenya), Lydia Ludic (Burundi) na Port (Djibout).

Kundi C ni St. George (Ethiopia), Dakadaha(Somalia), Yanga na Simba za Tanzania.

Spoti Mikiki ilifanya mahojiano na Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Masharikina Kati (Cecafa), Nicholas Musonye.

Swali: Cecafa mmekuwa kimya kwa kipindi kirefu, nini changamoto mlizokumbana nazo?

Musonye: Kuna watu tuliwabaini walikuwa wanaturudisha nyuma kwa hiyo tumeamua kuachana nao ili tuendelee kupiga hatua, kama inavyofahamika tayari tuna uongozi mpya ni vyema kuupa nafasi ya kuona ni vitu gani vizuri ambavyo vipo mbele.

Swali: Mpango wa Cecafa ni upi hasa kujijenga kiuchumi?

Musonye: Tumepita kwenye kipindi kigumu. Tumekuwa tukipanga mambo mbalimbali lakini tunakwama kiuchumi na zaidi ni kukosa udhamini. Lakini pamoja na hayo, udhamini wa Azam ambao wamepata haki za kurusha matangazo ya moja kwa moja kwa njia ya Television, umesaidia kwa kiasi chake kwenye kuandaa haya mashindano.

Swali: Kwanini wadhamini wamekuwa wa kuvuta kwa kamba?

Musonye: Inawezekana ni hali ya kiuchumi, lakini pia gharama za kufanya mashindano ni kubwa, tukisema tuwaachie hawa wadhamini wawili pekee hatutoweza kufikia malengo.

Swali: Nini mkakati wenu wa kupata wadhamini zaidi?

Musonye: Niseme tu bado milango ipo wazi kwa wadhamini wengine kuja kuongeza nguvu, kwa sababu lengo ni moja kuona Cecafa inapiga hatua.

Swali: Huoni kuna haja ya wewe kuwajibishwa kwa kukosa kufanya mashindano mara kwa mara?

Musonye: Kama nilivyosema, tatizo ni wafadhili, lakini kama zikipatikana, mashindano yatafanyika kama kawaida.

Swali: Vipi kuhusu wahujumu wa baraza hili?

Musonye: Kuna matatizo mengi, lakini tunadhani sasa wakati umefika kwa kila atakayekuwa analihujumu baraza atakuwa akiwajibishwa ili yaliyotokea kwa kipindi cha miaka miwili nyuma bila ya mashindano hayo yasijirudie.

Swali: Kama Cecafa, mna mipango gani endelevu?

Musonye: Kuhusu mipango endelevu, tunajipanga kuona kuwa Cecafa inakuwa na uwezo wa kuandaa mashindano mbalimbali bila ya kutegemea wahisani pamoja na mfumo wa uendeshaji wa mashindano hayo.

Swali: Nini mikakati ya uongozi mpya kwa sasa?

Musonye: Uongozi mpya utatengeneza mikakati ya kuhakikisha wanakuwa na mifumo mizuri pamoja na kuboresha zaidi ligi hiyo lakini hilo pamoja na mengine mengi ni mambo ambayo yapo chini ya uongozi mpya.

Swali: Kuna mipango yoyote ambayo Cecafa inataka kuleta kama mambo mapya ya uongozi mpya?

Musonye: Mabadiliko yanahitaji muda kwa hiyo, kuna kazi mbele ya kufanywa na uongozi mpya na mengi yameanza kujadiliwa kwenye vikao vilivyopita, tutayaweka wazi.