In Summary
  • Asilimia kubwa ya vijana wanaochipukia kwenye soka wanatamani kufikia mafanikio ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba mwenye tuzo mikononi mwake ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani ambayo aliitwaa 2015.

Ukweli usiopingika ni kwamba, nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ‘Samagoal’ anayeichezea, KRC Genk ya Ubelgiji amekuwa mfano mzuri wa kuingwa na vijana wengi wanaochipukia kwenye soka la Tanzania.

Asilimia kubwa ya vijana wanaochipukia kwenye soka wanatamani kufikia mafanikio ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba mwenye tuzo mikononi mwake ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani ambayo aliitwaa 2015.

Haikuwa lele mama kwa Samatta kutwaa tuzo ya Afrika na mpaka kufikia hatua ya kucheza soka barani Ulaya, wapi alipatia nahodha huyo wa Taifa Stars kwenye uchezaji wake soka?

Spoti Mikiki inakuletea mambo matano yaliyomtengeneza Samagoal na ndiyo maana leo hii amekuwa mfano mzuri kwa wachezaji wengi wa Tanzania na hata Afrika Mashariki na Kati.

Menejimenti

Samatta yupo chini ya Kampuni ya Sportbank ambayo imesambaa kwenye mataifa mbalimbali ndani na nje ya Afrika, kampuni hiyo ambayo pia ofisi zake zipo, Ubelgiji imeweka wazi majukumu yake kuwa ni kusimamia ndoto za wachezaji, makocha na kushauri wazazi kwenye masuala ya soka.Sehemu ya mafanikio ya mchezaji yeyote ni kuwa chini ya watu makini, ukiachilia mbali Samatta kuwa chini ya Kampuni hiyo pia baba yake mzazi, Mzee Ally pamoja na washauri wake wa karibu wamekuwa msaada mkubwa kwa nyota huyo na zaidi ni usikivu.Hilo ni eneo kubwa ambalo Samatta amefanikiwa tofauti na wachezaji wengi wa ndani ambao wamekuwa kwenye mikono ya wapigaji ambao hawatazami malengo ya mchezaji na hupenda kujitizama wao wenyewe ili kujinufaisha kwa kupata cha juu.

Hakuchezea nafasi

Wakati wawakilishi wa TP Mazembe wanatua nchini kwa ajili ya kumnasa Samatta mwaka 2011, mshambuliaji huyo hakuingia mitini kwenye dili hilo kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma ambacho ilitajwa Mrisho Ngassa aliingia mitini pindi ambapo vigogo wa Al-Merrikh SC walipotua.

Uamuzi sahihi

Kutochezea kwake nafasi kulimfanya kuwa sahihi kwenye uamuzi wa kujiunga na TP Mazembe, usahihi wake ni kwenye umri ambao alikuwa nao kwa kipindi hicho.

Samatta ambaye kwa sasa ana miaka 25 aliondoka Simba akiwa na miaka 18, hicho kilikuwa kipindi sahihi kwake kuanza kukabiliana na changamoto mpya za soka sehemu nyingine kabla ya kutua Ulaya.

Kujitambua

Samatta ni miongoni mwa wachezaji wachache wa Kitanzania ambao wanajitambua kwenye hilo, mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon kabla ya kujiunga na Simba amekuwa na mlolongo mzuri wa historia yake ya soka, inayomfanya kuwa na mafanikio ya hali ya juu.

Kujituma

Juhudi zake zilimfanya kuwa bora na kujiwekea ufalme wake nchini DR Congo , Samatta aliiongoza TP Mazembe kutwaa mataji saba kwa kipindi cha miaka mitano aliyoitumikia klabu hiyo.

Mataji hayo ni kombe la Ligi Kuu ‘Linafoot’ nchini humo mara nne kwenye miaka ya 2011, 2012, 2013, 2014, Super Coupe du Congo mara mbili katika miaka ya 2013, 2014 na Ligi ya

Mabingwa Afrika mara moja.

Samatta alijituma na ndio maana alifanikiwa kuwa mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani mara baada ya kuiwezesha Mazembe kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015. Alisajiliwa na KRC Genk kwa dau la Dola800,000 ikiwa ni msimu wake wa tatu klabuni hapo.