In Summary
  • Wafanyakazi wengi hutegemea kupata huduma hizi za kifedha kama kuweka akiba, kuhamisha fedha na kupata mikopo kutoka kwenye taasisi binafsi.

Moja ya changamoto inayowakumba wafanyakazi wa Tanzania ni upatikanaji wa huduma za kifedha kwa bei nafuu na kwa haraka.

Wafanyakazi wengi hutegemea kupata huduma hizi za kifedha kama kuweka akiba, kuhamisha fedha na kupata mikopo kutoka kwenye taasisi binafsi.

Taasisi hizi binafsi zinazongozwa na wafanyabiashara ambao lengo lao kubwa ni kupata faida. Shauku hii ya kupata faida humuumiza mlaji, ambaye analipishwa gharama kubwa kwa kila huduma anayoipata.

Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (Saccos) ni asasi za kifedha zinazoanzishwa, kumilikiwa na kuongozwa na wanachama kwa misingi ya kidemokrasia ili kuwasaidia kujifunza kuweka akiba na kuweza kupata mikopo kwa riba nafuu kutokana na akiba zao.

Ijapokuwa kumekuwa na changamoto kadhaa kwenye uendeshaji wa baadhi ya vyama hivi, bado hauwezi kudharau umuhimu wake kwenye kumsaidia mfanyakazi aweze kupata huduma za kifedha kwa bei nafuu.

Baadhi ya Saccos kubwa na zenye mafanikio zaidi nchini ni zile zilizoanzishwa na wafanyakazi. Saccos siyo biashara ya mtu mmoja, humilikiwa na wanachama kwa ujumla wao.

Uzuri wa Saccos ni kwamba, mmiliki na mteja ni mwanachama huyohuyo, kwa sababu hiyo inakuwa rahisi kwake kujipatia huduma kwa bei ambayo haitamuumiza.

Wafanyakazi wakijiunga kwa pamoja kwenye taasisi yao, wanaweza wakaanzisha Saccos. Na kwa sababu wao wenyewe ndiyo wamiliki inakuwa rahisi kujitengenezea kanuni na masharti yatakayokuwa yanawasaidia kwenye urahisi wa kujipatia huduma za kifedha.

Kutokana na sheria ya Ushirika ya mwaka 2013, Saccos inaweza kuanza ikiwa na wanachama wasiopungua 20.

Zifuatazo ni faida ambazo wafanyakazi watazipata kama wanaweza kuanzisha Saccos kwenye mazingira ya kazini.

Unajifunza kuweka akiba

Unapokuwa mwanachama wa Saccos wajibu mmojawapo wa msingi ni kuweka akiba. Kwa sababu ni kutoka kwenye akiba hizo ndipo chama kinapata fedha za kukopesha

Mwanachama anaweza kukopa mara tatu ya kiasi cha akiba aliyo nayo. Hivyo, utalazimika kuweka akiba ili uweze kupata huduma ya mikopo. Pia, kwa sababu ya msisitizo wa kuweka akiba, unatolewa na viongozi wa Saccos inakulazimisha kuwa na tabia ya kujiwekea akiba.

Baadhi ya wanachama wa Saccos wamekubaliana kukatwa kiasi cha fedha kutoka kwenye mishahara yao kila mwezi ili kiende kwenye akiba. Hivyo unachokipokea mwisho wa mwezi tayari kimeishakatwa akiba.

Akiba hizi ni mali ya wanachama, uanachama wako ukiisha kwa sababu yoyote, unaweza kuichukua.

Kwenye vyama vingi vya Ushirika wa Akiba na Mikopo unaweza kuweka fedha yako kama akiba na kuichukua wakati wowote na bila kulipishwa gharama za kuitunza fedha hiyo.

Hii ni tofauti na huduma zinavyotolewa kwenye taasisi nyingi za kifedha, ambazo ukiweka fedha kwenye akaunti yako wakati wa kuja kuichukua utalipia gharama ya kuitoa.

Ukiweka Sh200,000 kwenye akaunti yako benki, wakati wa kuitoa unaweza ukatoa Sh195,000 tu.

Unaweza kukopeshwa kwa riba nafuu na bila masharti magumu.

riba ni kiasi cha fedha anayolipa mkopaji juu ya mkopo halisi. Kiasi hiki cha fedha ndiyo faida anayoipata mkopeshaji kutokana na uwekezaji aliyoufanya.

Ijapokuwa ni muhimu Saccos zipate faida ili ziweze kujiendesha, lengo kuu siyo kupata faida. Hii ndiyo sababu Saccos inaweza kuwa na riba nafuu ukilinganisha na asasi zingine. Kwa sababu anayeamua kiasi cha riba ni mkopaji, atajipangia kiasi ambacho ni himilivu na masharti atakayoyaweza.

Taasisi nyingi za fedha zimekuwa na masharti magumu kwenye upatikanaji wa mikopo. Muombaji wa mkopo anapewa fomu nyingi za kujaza, na kuambiwa alete viambatanisho vingi na wakati mwingine unatakiwa uwe na dhamana ya mali isiyohamishika.

Haimaanishi kwenye Saccos hakuna fomu nyingiza kujaza, ila kuna fomu ambayo kuijaza kwake ni rahisi na masharti yake ni nafuu. Kunaweza kusiwe na kiambatanisho chochote kinachohitajika, au ukatakiwa kuambatanisha hati ya mshahara tu.

Siyo jambo la kushangaza kwenye chama cha ushirka wa akiba na mikopo kujaza fomu ya kuomba mkopo asubuhi, halafu mchana ukapigiwa simu kuwa mkopo wako uko tayari. Hii ni tofauti na taasisi zingine za kifedha ambazo unaweza kuusubiri mkopo uliouomba kwa mwezi mmoja hadi miwili.

Ni rahisi kupata fedha unapokumbwa na dharura

Kwenye maisha kuna mambo yanayotukuta wanadamu kama maradhi, misiba ambayo hatukuyatarajia wala hayakuwapo kwenye bajeti zetu. Yanapokukuta mambo kama haya, ukihitaji mkopo kwenye Saccos taratibu zake zinakuwa rahisi zaidi na mkopo unapatikana kwa haraka.

Haihitaji ushahidi wowote ili kudhibitisha kwamba una dharura, hata kama ni nyumba yako unataka ukaimalizie kwa dharura, ili mradi wewe ni mwanachama na una vigezo sitahiki utapatiwa mkopo kwa dharura.

Saccos inakutunzia heshima, kwa kukuepusha kuanza kuelezea matatizo yako kwa kila mtu ili akukopeshe fedha. Wakati wa dharura huwezi kuwategemea watu binafsi, kwa sababu siyo mara zote wataweza kukusaidia.

Wakati mwingine unaweza kupata mtu wa kukusaidia ila utatakiwa kuilipa fedha hiyo kwa kipindi kifupi au utalipishwa riba kubwa.

Utakapostaafu utakupata fedha ya kuanzia maisha

Nimesikia mara kadhaa wastaafu wakilalamika kuhusu ucheleweshwaji wa pensheni zao. Baada ya kustaafu wanarudi mtaani wanasubiri miezi kadhaa kabla ya kuanza kulipwa.

Kama utastaafu ukiwa mwanachama wa Saccos utarudishiwa kiasi chako cha fedha ulichowekeza kama hisa na akiba. Fedha hii hulipwa pale tu uanachama wa muombaji umefika mwisho.

Kwa sababu mchakato wake wa kuzipata ni rahisi, huwa hazichelewi kulipwa. Ile miezi ya kusubiri pensheni ianze kulipwa hautakosa fedha za matumizi.

Gidion Obeid ni Mhadhiri wa Uhasibu na Usimamizi wa Fedha, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na mwanafunzi wa Shahada za Uzamivu (PhD). Kwa ushauri wasiliana naye kwa namba 0625698050