In Summary
  • Licha ya kuwa gesi ni rafiki wa mazingira na afya, takwimu zilizomo kwenye ripoti ya Energy Access Situation ya mwaka 2016 zinaonyesha ni asilimia 7.2 pekee ya kaya nchini ndizo zinazotumia nishati hiyo kama chanzo cha kupikia ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 0.3 iliyokuwapo 2011/2012.

Utumiaji wa gesi kama chanzo cha kupikia ni salama kwa afya, hutunza mazingira kwa namna zote tofauti na nishati ya mkaa na kuni ambazo zinapigwa vita hivi sasa.

Licha ya kuwa gesi ni rafiki wa mazingira na afya, takwimu zilizomo kwenye ripoti ya Energy Access Situation ya mwaka 2016 zinaonyesha ni asilimia 7.2 pekee ya kaya nchini ndizo zinazotumia nishati hiyo kama chanzo cha kupikia ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 0.3 iliyokuwapo 2011/2012.

Wakati idadi ya kaya zinazotumia gesi kama chanzo cha kupikia zikiongezeka uingizwaji wake pia umeshuhudiwa kuongezeka katika siku za hivi karibuni kwa mujibu wa Ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) ya 2017.

Katika mwaka wa fedha 2015/16 na 2016/17 ongezeko la asilimia 50 lilirekodiwa ikiwa ni mara 16 ya ongezeko la asilimia 3.12 lililokuwapo katika mwaka wa fedha 2014/15 na 2015/16.

Mwaka 2016/17 kiasi cha futi za ujazo 107,083 ziliingizwa nchini ikilinganishwa futi za ujazo 71,311 zilizoingizwa 2015/16.

Ongezeko hilo lilichangiwa na kampeni zinazofanywa na mamlaka husika kuhusu matumizi ya gesi ambayo ni pamoja na kuongeza mikakati ya kimasoko iliyofanywa na kampuni za uingizaji gesi hiyo.

“Lakini pia katika kipindi hicho, mamlaka ilishuhudia kuongezeka kwa uuzaji wa gesi hiyo nchini Kenya jambo ambalo huenda ndilo lililochangia kuongezeka kwa uingizwaji wake nchini,” ripoti ya Ewura ya 2017 inabainisha.

Akizungumzia hali hiyo, mkurugenzi wa mikakati ya utafiti wa Repoa, Dk Abel Kinyondo anasema ongezeko la uingizwaji wa gesi hiyo unaweza kuwa umechangiwa na uamuzi wa watu kutaka kuachana na nishati za asili za kupikia na kuhamia katika njia za kisasa. “Katika majiji na mikoa inayoendelea bei ya gunia la mkaa ni karibu mara mbili ya bei ya mtungi wa gesi huenda hiyo ikawa ni sababu ya watu kuamua kubadilika na kutumia gesi katika kupikia,” anasema Dk Kinyondo.

Anasema hivi sasa inaonekana watu wengi wanaweza kuimudu gharama jambo ambalo linawafanya waachane na mkaa ili kutafuta unafuu wa maisha.

“Lakini ni miaka mingi sasa imepita tangu kugunduliwa kwa gesi ya Songosongo tena nyingi kwanini uingizwaji wa gesi usingepungua na badala yake unazidi kuongezeka,” alihoji Dk Kinyondo.

Gharama

Hata hivyo, utumiaji wa gesi kwenye kupikia umeonekana kuwa na unafuu kwa baadhi ya watu kutokana na kupunguza matumizi ya fedha kama ilivyokuwa kwa Ruth Nzyungu mama wa watoto wanne ambaye alikuwa akitumia Sh2,000 kila siku kununua mkaa ambayo ni sawa na Sh60,000 kwa mwezi mzima.

“Japo bado natumia mkaa kuchemsha vitu vigumu kama maharagwe, njugu mawe lakini gharama zimepungua kwa sababu sasa hivi nikijaza gesi Sh20,000 na mkaa Sh10,000 natumia kwa mwezi mzima na ninakua nimeokoa Sh30,000,” anasema Ruth.

Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida, watumiaji wengi wa gesi wanapatikana katika maeneo ya mijini huku asilimia 71.2 ya watu waishio vijini bado wanatumia kuni kama nishati ya kupikia.

Mikoa inayoongoza kwa matumizi ya gesi ni Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Kilimanjaro, Mbeya na Manyara.

Katika jiji la Dar es salaam takwimu zinaonyesha asilimia 26.7 ya wakazi wanatumia gesi kama nishati ya kupikia, Mafuta ya taa(22.1), kuni (14.3) mkaa (88.2) huku Mkoa wa Simiyu ukitajwa kuongoza katika matumizi ya kuni kwa asilimia 94.3.

“Hata kama majiko ya umeme na gesi yanauzwa kwa bei ya chini, wengi tunaogopa athari tunazoweza kuzipata kutokana na kutojua namna nzuri ya kuyatumia na kukosa elimu inayojitosheleza,” anasema Rose Kajula (43) mkazi wa Buguruni Malapa.

Anasema ununuaji wa gesi unahitaji mtu kuwa na kipato cha kuweza kumudu gharama za manunuzi tofauti na mtu anayetumia mkaa au kuni.

Anasema matumizi ya gesi si makubwa kutokana na bei kubwa za uuzwaji zilizopo jambo ambalo linamtaka mtu kuwa na kipato angalau kinachomuwezesha kumudu gharama za manunuzi ya mara moja.

“Unajua unaponunua gesi ni tofauti na mkaa au kuni, mkaa unanunua Sh1,500 au Sh2,000 kwa siku, sawa ni kubwa ukijumlisha kwa mwezi lakini unapotaka kununua gesi ni lazima uwe na fedha taslimu 21,000 ndipo upewe, nitaweza wapi wakati mimi maisha yangu ya kuunga unga,” anasema Rose.

Kauli ya Rose inaungwa mkono na muuzaji wa gesi ya kupikia katika eneo la Mtoni Kijichi jijini Dar es Salaam, Yohana Charles anasema licha ya kuwa uingizwaji wa gesi ya kupikia nchini umeongezeka, gharama za uuzaji wa gesi hiyo bado uko juu.

Hivi sasa bei ya mtungi wa gesi wa kilo 15 ni Sh49,000 ambayo imepanda kutoka Sh45,000 mwaka uliopita huku mtungi wa Kilo 6 ukiuzwa kwa Sh19,000 kutoka Sh18,000 iliyokuwapo mwaka uliopita.

Anasema jambo hilo limechangia mauzo yake kushuka hadi kufikia mitungi mitatu kwa wiki ikilinganishwa na mitungi minane aliyokuwa akiiuza mwaka uliopita na hiyo inatokana na bei yake kuwa ndogo kwa wakati huo.

“Kwa upande wetu biashara ni ngumu, japo uingizaji unaongezeka lakini tunalazimika kuuza kwa bei ya juu ili kuhakikisha tunapata faida huku idadi ya wateja ikipungua,” anasema Charles.

Ripoti ya EASR 2016 imeitaja gesi kama chanzo cha kupikia chenye gharama kubwa kwa wastani wa Sh31,874 kwa mwezi ikifuatiwa na mkaa kwa Sh30,611 huku mafuta ya taa yakitajwa kama chanzo rahisi ambacho matumizi yake kwa mwezi ni wastani wa Sh18,156 pekee.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa wakala wa Serikali wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja (PBPA), Erasto Simon anasema ni ngumu kuweka bei elekezi kwenye uuzaji wa gesi kutokana na kila msambazaji kuagiza kulingana na mahitaji yake na inapoingizwa nchini, huuza kutokana na bei aliyonunulia.

“Kama nchi bado hatujawa na uwezo wa kununua gesi nyingi kwa pomoja na kuwauzia wasambazaji wa ndani kutokana na uwezo wetu mdogo wa kuhifadhi mzigo mkubwa unaoweza kutosha wasambazaji wote nchini,” anasema Simon.

“Tuko mbioni na hivi karibuni kampuni ya Orxy na Mihan tayari wameanza kufanya hivyo ili kuhakikisha wanakuwa na bei moja kusudi kuweka urahisi kwa wanunuaji,” anasema.

Meneja mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo anasema ni mapema sana kuanza kutangaza bei elekezi kwa wauzaji wa gesi kutokana na soko kuwa bado changa.

“Pindi tutakapo jiridhisha kuwa soko limechangamka tutaweka bei elekezi kwa wauzaji hao ambayo watatakiwa kuifuata,” anasema Kaguo.

Lakini huenda tangazo la kufikia ukomo wa matumizi ya mkaa Juni Mosi 2017 kulichangia kwa kiasi kikubwa uingizwaji wa gesi ya kupikia nchini na kufanya watu wapunguze matumizi ya mkaa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos anasema moja ya changamoto iliyokuwa ikifanya watu wasibadili matumizi ya mkaa ni upatikanaji wa nishati mbadala ya kupikia kwa uhakika na gharama nafuu tofauti na ile waliyoizoea.

“Kama ni gesi basi ipatikane karibu na nyumba zao na hivi karibuni tulifanya kampeni nyingi ikiwamo ya kutangaza kuzuia matumizi ya mkaa Juni 2017, jambo ambalo lilichangia watu wengi kutafuta mbadala wa nishati ya mkaa ili kuepuka kuathirika na hatua ngumu zinazoweza kuchukuliwa,” anasema Santos.

Endapo uingizwaji wa gesi utaongezeka, itakuwa ni ahueni kwa misitu kwa sababu kitu kilichokuwa kikiweka changamoto katika kupiga vita matumizi ya mkaa ni kukosekana kwa nishati mbadala ya uhakika.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, jumla ya tani milioni tano za mkaa huzalishwa nchini kila mwaka zinatokana na ukataji wa misitu.

Mkurugenzi wa Sekta binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye anasema ongezeko la uingizwaji wa gesi ni habari njema pia ni ishara ya kuwa matumizi ya nishati ambazo zinaharibu mazingira utaanza kupungua na watu watahamia katika nishati ambazo ni rafiki wa mazingira

“Hata uzalishaji viwandani sasa utaongezeka kwa sababu vitaweza kuhamia katika matumizi ya gesi kuendesha shughuli zake za kila siku.

“Japo hata sasa baadhi ya washiriki wetu wanadai hali ya biashara imeanza kutengemaa baada ya watu kulalamika sana na kuamua kuiga namna ya kuishi ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano,” anaongeza.

Lakini kama nchi ina gesi ya asili kiasi cha futi za ujazo trilioni 57 katika eneo la Songosongo ambayo inatosha kwa matumizi ya nchi nzima lakini mpaka sasa ni nyumba 30 pekee ndizo zilizoweza kuunganishwa katika mradi wa majaribio huku nyumba nyingine 150 zikitarajia kuunganishwa katika mkoa wa Dar es Salaam kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Kapulya Musomba aliwahi kunukuliwa na gazeti hili akisema ujenzi holela wa nyumba katika baadhi ya miji umekuwa ni chanzo cha ucheleweshaji usambazaji wa gesi ya asilia majumbani.

“Kwa kulitambua hilo, Ni vyema sasa mipango miji watakapo kuwa wanahitaji kuandaa ramani wakatushirikisha na sisi ili tuweze kuweka ramani madhubuti itakayotupatia urahisi katika kupitisha mabomba yetu ili kuwafikia wakazi wa majumbani,” anasema Musomba.

“Jambo hili limekwamisha kwa kiasi kikubwa katika kufikia adhma tuliyokuwa tumejiwekea ya kuweza kusambaza gesi katika nyumba 30,000 ndani ya mwaka mmoja na badala yake mpaka sasa ni nyumba 70 ndiyo zimefikiwa,” alisema Musomba