In Summary
  • Uchumi wa Tanzania unategemea sana kilimo. Zaidi ya theluthi mbili ya Watanzania wanategemea kilimo na zaidi ya asilimia 80 wanajihusisha nacho. Changamoto iliyopo ni udhibiti wa mapato yanayotokana na kilimo. Baada ya mkulima kutoa jasho shambani, anapovuna wanaonufaika zaidi yake ni wengi.

Nadhani ni nadra sana kumpata Mtanzania asiyefahamu kilimo manufaa ya kilimo. Wengi wanafahamu na wanashiriki kwenye mnyororo wake wa thamani.

Lakini, ili taasisi yoyote iweze kujitegemea na kutoa huduma bora, inahitaji vyanzo vya uhakika vya mapato. Inaweza kuwa ni kutokana na kodi, ushuru wa bidhaa au huduma, mikopo au misaada. Vyovyote iwavyo, fedha inahitajika kufanikisha mipango yake.

Kila mkoa nchini una chanzo cha uhakika cha mapato. Ipo inayozalisha kahawa, korosho, tumbaku, pamba, katani, alizeti na mazao ya chakula. Mikoa mingine inachimba madini ya aina tofauti. Leo tuzungumzie inayolima pamba ambayo mingi inapatikana kanda ya ziwa.

Kwa miaka mingi mikoa ya kanda ya ziwa imejengwa kwa mapato yatokanayo na uzalishaji wa pamba. Baadhi walilibatiza zao hili na kuliita ‘dhahabu nyeupe.’

Takwimu zinaonesha Mkoa wa Shinyanga kabla ya kugawanywa na kuipata Simiyu na Sinyanga, ulikuwa unazilisha asilimia 40 ya pamba yote nchini. Pamoja na kiwango kikubwa cha uzalishaji, kasi ya kupunguza umasikini na kutengeneza ajira ipo chini.

Pamoja na changamoto ya wakulima wa pamba kuzalisha bila kufuata kanuni na maelekezo, wafanyabiashara nao wameonekana kuneemeka kupitia udanganifu wanaowafanyia wakulima.

Changamoto kubwa ya wakulima imekuwa ni kuchanganya pamba na mazao mengine ikiwemo mahindi, maharage, kunde au alizeti. Mchanganyiko wa pamba na mazo mengine unatajwa kuhatarisha afya za walaji wa mazao yaliyochanganywa kutokana na aina ya dawa zinazonyunyizwa kwenye pamba kuilinda na wadudu waharibifu.

Hata baada ya mavuno, baadhi ya wakulima wamekuwa na kawaida ya kuchanganya pamba na mchanga au maji kwa lengo la kuongeza uzito. Udanganyifu huu unapaswa kuachwa mara moja kwani hupunguza thamani na ubora wa zao hilo kwa kiasi kikubwa.

Baadhi ya wafanyabiashara wana utamaduni wa kununua pamba kutoka kwa wakulima kwa kutumia vipimo ambavyo havijathibitishwa na Serikali. Pia wapo wanaotumia mizani zisizo na viwango ili kumpunja mkulima jambo linalovua vita kwa kila upande kutaka kumuwahi mwenzake.

Kuviziana huku kati ya wakulima na wafanyabiashara wasio waaminifu kunakosababisha kufifisha ubora na thamani ya pamba kunazikosesha halmashauri za mikoa inayolima zao hilo mapato inayostahili yatokanayo na ushuru wa asilimia tatu kwa kila kilo moja inayouzwa.

Kwa mtazamo wangu, ili kuongeza mapato yatokanayo na ushuru wa pamba, wanasiasa wanapaswa kuwaacha watendaji wa Serikali kusimamia na kutekeleza sheria, taratibu, kanuni, miongozo, maelekezo na maazimio yanayohusiana na uzalishaji wa zao hilo.

Pili, kila Halmashauri iingie mkataba ‘makini’ na kampuni zinazokusudia kununua pamba katika maeneo yao. Kila kampuni ipewe kibali cha kukunua pamba kwa kiasi ilicholipia malipo ya awali. Kwa mfano, kampuni Y inatarajia kununua tani elfu 20 kutoka halmashauri X uwe ni wajibu wa kampuni kulipia sehemu ya tani elfu 20 kabla ya kuingia sokoni.

Baada ya kiasi kilicholipiwa kununuliwa, kampuni hiyo irudi halmashauri kuomba kibali kipya cha kununua kiasi kingine inachohitaji. Lengo ni kudhibiti takwimu za ununuzi ili kutoza ushuru halali utakaochangia kukuza mapato ya halmashauri hivyo kuweka mipango sahihi ya kuendeleza kilimo cha zao hilo.

Sual ajingine m,uhimu ni kila halmashauri kuwa na kikosikazi maalumu kwa ajili ya kufuatilia mwenendo mzima wa uuzaji na ununuzi wa pamba. Kikosikazi hiki ni lazima kiwezeshwe kwa vifaa madhubuti yakiwamo magari na mafuta ya kutosha, posho za watumishi watakaoteuliwa na ni vyema kikashirikisha walinzi wa raia na mali zao hasa nyakati za usiku.

Ni vyema kikosi kazi maalum kikawa na utaratibu wa kubadili wajumbe kila baada ya muda ili kuepuka kuzoeleka na kupunguza mianya ya rushwa. Uongozi wa halmashauri unapaswa kuwa na ratiba ambayo haitakuwa rahisi kueleweka miongoni mwa wafanyabiashara wenye nia ya kufanya ujanjaujanja.

Nne, kila Halmashauri izuie usafirishaji wa pamba baada ya saa 12 jioni. ili kudhibiti magendo ambayo ni rahisi kufanyika nyakati za usiku. Vilevile, watendaji wa kata, vijiji na wataalam wa kada mbalimbali kwenye maeneo hayo wanapaswa kushirikishwa kwenye juhudi hizi za kuimarisha mfumo na kudhibiti upotevu wa mapato katika maeneo yao.

Kubwa zaidi kuelekea uchumi wa viwanda, kila halmashauri inayozalisha pamba ibuni kiwanda kitakachotumia malighafi ya zao hilo ili kupunguza usafirishaji wa pamba ghafi hivyo kukuza ajira kwa vijana na kupunguza umasikini. Aidha, wadau wote washirikiane kuhakikisha pamba inazalishwa kwa wingi zaidi.

Hapa, taasisi na bodi zenye dhamana ya kusambaza mbolea na viuatilifu zinapaswa kufikisha mahitaji hayo kwa wakati