In Summary
  • Meli zilizokuwa maarufu enzi hizo ikiwemo Messina Linea ya Italia na wazamiaji walikuwa hawakauki bandarini na zinapotia nanga hutumia ujanja wao na kuingia kwenye meli hizo na kuzamia Ulaya kupitia Afrika Kusini.

Mwishoni mwa miaka ya 1970 na miaka ya 1980, Waafrika wengi walikimbilia Ulaya kutafuta maisha kwa kile walichodai hali ngumu. Wapo waliodiriki kuteka hata ndege waende Ulaya, wapo waliokuwa wakishinda bandarini kwenye nchi zenye bandari kusubiri meli ili wazamie.

Meli zilizokuwa maarufu enzi hizo ikiwemo Messina Linea ya Italia na wazamiaji walikuwa hawakauki bandarini na zinapotia nanga hutumia ujanja wao na kuingia kwenye meli hizo na kuzamia Ulaya kupitia Afrika Kusini.

Hata mchezaji wa Denmark, Yussuf Yurary Poulsen, baba yake alizamia melini na kupata kazi huko katika meli ya makontena, sasa alipotua Denmark akampata mama yake ambaye ni raia wa huko. Baba wa Poulsen alikuwa Mdigo wa Chumbageni, Tanga.

Sasa, ukiangalia mechi ya nusu fainali ya Ufaransa na Ubelgiji wengi wa wachezaji wake, wazazi wao walikuwa wahamiaji kutoka Afrika.

Itakumbukwa mwaka 2002, liliwahi kupigwa zengwe kwamba Ufaransa haionyeshi kama Wafaransa halisi na hata Rais wa wakati huo, Jacques Chirac wakati wa kampeni zake aliwahi kusema atahakikisha anarudisha sura ya Ufaransa timu ya taifa kwani ilikuwa imejaa weusi watupu.

Wakati fainali za Kombe la Dunia zikiendelea huko Russia, huku Ulaya suala la wazamiaji kutoka Afrika limekuwa gumzo dunia nzima kiasi cha Italia, Hispania na Ujerumani kutangaza utaratibu wa kuwapokea wazamiaji hao kutoka Afrika na sasa limekuwa suala la kisiasa zaidi. Wengi wa wazamiaji wanatoka Afrika Kaskazini na Magharibi.

UFARANSA

Uwepo wa wazamiaji kutoka Afrika, sura ya timu ya Ufaransa na liliwahi kukuzwa kisiasa zaidi kwani itakumbukwa pia wakati wa kampeni za Ufaransa mwaka jana, Emmanuel Macron, alisema anataka kuifanya Ufaransa iwe ya Wafaransa halisi kwa kuwa akiiangalia Ufaransa ‘Les Bleus’, hajaielewa bado kama ni Ufaransa hasa anayoifahamu.”

Hata hivyo, wachezaji wa Ufaransa wenye asili ya Afrika wameibeba Ufaransa kwa kiasi kikubwa kama ilivyo kwa mshambuliaji wake, Kylian Mbappe ambaye amezaliwa Ufaransa lakini wazazi wake wote wanatoka Afrika. Ni wahamiaji. Baba yake ni raia wa Cameroon wakati mama yake ni raia wa Algeria ambao walikutana huko Paris, Ufaransa na kumzaa staa huyo.

Mbappé akiwa na miaka 17 ameonyesha soka ya kiwango, kiasi cha kuwaadhibu wakongwe Argentina kwa kusababisha mabao matatu katika mechi yao ya 16 Bora.

Wakati wa Fainali za Paris mwaka 1998, wengi wa wachezaji wa Ufaransa walikuwa weusi na walitwaa Kombe la Dunia.

Wafuatao ni wachezaji wa Ufaransa wenye asili ya Afrika ambao wazazi wao walifika Ufaransa ama kwa kuzamia au kwa ukimbizi wa kisiasa.

Samuel Umtiti na Adil Rami wanasimama kikamilifu kwenye ngome, wenyewe wana asili ya Afrika, Umtiti anatoka Cameroon wakati Rami asili yake ni Morocco.

Pia mchezaji tegemeo wa Ufaransa, Benjamin Mendy na Djibril Sidibe wana asili ya Afrika kwa kuwa wazazi wao walizamia Ufaransa wakitokea Senegal.

Kwa upande mwingine, yuko Presnel Kimpembe anayesimama na Umtiti na Rami ambaye naye ana asili ya DR Congo. Hao nao wanamlinda kipa, Steve Mandanda ambaye pia ana asili ya DRC.

Katika kiungo cha Ufaransa utawakuta; Paul Pogba, ambaye wazazi wake wanatoka Guinea. Pogba anashirikiana na mtu mmoja anaitwa Blaise Matuidi katika kiungo. Matuidi ana asili ya Angola na Congo.

N’Golo Kante, anayetawala dimba la kati asili yake ni Mali walikotoka wazazi wake.

Katika ushambuliaji yuko Ousmane Dembélé mwenye asili ya Senegal, Mali na kidogo Mauritania. Mashine ya mabao ya Lyon, yuko Nabil Fekir anayetokea Algeria.

UBELGIJI

Ubelgiji imeingia nusu fainali ya Kombe la Dunia unaweza kusema kama maajabu kwa kuitoa Brazil. Lakini haiwezi kushtua kwa kuwa Ubelgiji imepania kufanya maajabu.

Tukiiangalia Ubelgiji, nayo inajengwa na watoto wa wazamiaji waliotoka mataifa ya Congo, Morocco, Burundi, Mali. Ni timu ya tatu kwa ubora duniani na imeipiga Brazil mabao 2-1 na sasa inaisubiri Ufaransa kesho.

Ubelgiji ilijipanga kwenye soka yake. Ilitengeneza timu kwa kuanzisha program mbalimbali kuanzia ngazi ya watoto tangu mwaka 2000, msisitizo ukiwa kwenye ujuzi na ufundi kwa maendeleo ya soka kwa taifa.

Waliwatumia watoto wa wazamiaji kutoka Afrika kwa kuwatengenezea programu maalumu.

Hata hivyo, hawawaachi peke yao, wanawachanganya na wazungu na kuiita “golden generation”

Wanaitwa hivyo kwa kuwa kipindi chao cha kukua, huku ligi za Ulaya ziko katika ubora wake na huzitumia kuuza wachezaji lakini kwa kuanzia timu za nchini.

Ndiyo maana ukiangalia kwa undani sehemu kubwa ya wachezaji wa Ubelgiji wametoka ligi mbalimbali za Ulaya na ndiyo maana wanatisha.

Pia ukiangalia Ubelgiji, wachezaji wake wametoka mataifa ya Afrika, Romelu Lukaku ana asili ya DR Congo wakati Nacer Chadli ana asili ya Morocco sawa na Marouane Fellaini. Youri Tielemans naye ana asili ya DRC.

Kutokana na kuchanganya utamaduni wa kizungu na Afrika, Ubelgiji imekuwa kama Les Bleus na ilianza hayo miaka ya 1990 na baada ya miaka 10 inaelezwa kuwa weusi wamekuwa chachu ya mafanikio ya taifa hilo.

Red Devils kama ilivyo Ufaransa Les Bleus, itakuwa ngumu kuwatenganisha Wafaransa weupe na weusi au Wabelgiji weupe na weusi kwani kila mmoja ana mchango muhimu kwenye timu.

Wachezaji wenye asili ya Afrika ni pamoja na Vincent Kompany ambaye baba yake ni Mcongoman sawa na Dedryck Boyata ambaye naye alizaliwa Brussels, Ubelgiji. Kevin De Bruyne ni mzungu mwenye asili ya Afrika, Mama yake amechanganya lakini alizaliwa Burundi akaenda kuishi Ivory Coast. Mwaka 2013 De Bruyne alihojiwa akasema: “Mama yangu ana asili ya England lakini mimi ni Mbelgiji hasa.”

Marouane Fellaini, amezaliwa kwenye mji wa Brussels wazazi wake ni raia wa Morocco akiwa pamoja na mchezaji mwingine, Nacer Chadli.

— Youri Tielemans yeye ni chotara, baba yake ni mzungu lakini mama yake ni ana asili ya D.R. Congo sawa na Mousa Dembélé, baba yake ni raia wa Mali na mama yake Tilly Huygens, ni Mbelgiji.

Nacer Chadli alizaliwa kwenye mji wa Liege, Ubelgiji lakini wazazi wake wana asili ya Morocco na mwaka 2011 Nacer aliichezea timu ya taifa ya Morocco kabla ya kuamua kubadili uraia na kuichezea Ubelgiji. Dedryck Boyata naye ni Mcongoman aliyezaliwa

Brussels.

Sehemu kubwa inaonekana, watoto wa wazamiaji kutoka Afrika Magharibi na watoto wa wazamiaji kutoka DR Congo nani zaidi? Ni suala la kusubiri muda tu kuona nani atafanya kucheza fainali za mwaka huu.