In Summary
  • Kuna walioziona kama sehemu nyingine ya siasa za siku hizi au sehemu ya wapinzani kujipenyeza kwa njia ya nyaraka za maaskofu.

Nyaraka za maaskofu wa KKKT na TEC, zimeleta changamoto kwenye jamii yetu. Zilipotolewa, yalisemwa mengi, kuna waliounga mkono na waliozipinga.

Kuna walioziona kama sehemu nyingine ya siasa za siku hizi au sehemu ya wapinzani kujipenyeza kwa njia ya nyaraka za maaskofu.

Lakini, waumini wa kweli waliziona kama nyaraka za maaskofu wanazozitoa wakati wa sikukuu na pale inapolazimika. Vyovyote vile, ujumbe wa maaskofu si wa serikali.

Tukio la barua ya serikali ambayo sasa hivi imeelezwa na Waziri wa Mambo ya ndani Dk Mwigulu Nchemba kuwa batili, umechochea changamoto zilizoibuliwa na nyaraka za maaskofu.

Kama kweli maaskofu wa KKKT, waliitwa na Msajili wa vyama vya kijamii na mashirika ya kidini na kufanya naye mazungumzo juu ya barua hiyo, hakuna jinsi serikali inavyoweza kukana kuifahamu.

Vinginevyo, tuambiwe kwamba waziri mkuu, hafahamu yale yanayoendelea siku kwa siku kwenye wizara mbalimbali au mawaziri hawafahamu chochote kinachoendelea mpaka mambo kiandikwe kwenye magazeti na mitandao. Kwa maneno mengine hakuna uratibu na mawasiliano kwenye serikali.

Vyovyote vile, ni muhimu Watanzania wakatambua kwamba kuandika waraka kwa waumini ni kazi ya maaskofu, na kwa kufanya hivyo hawahitaji ruhusa ya serikali na hasa kama ujumbe wao unahusu maisha ya kiroho.

Ingawa sina nia ya kuwapinga maaskofu wetu, binafsi nina mtizamo tofauti kidogo juu ya nyaraka hizi, ni mtizamo wa kujenga na wala si wa kubomoa: Nyakati hizi tunahitaji mifumo na si waraka.

Mfumo tunaoutaka

Tunahitaji mifumo yenye kuelekeza maadili mema, isiyokuwa na ubaguzi wala matabaka. Mifumo isiyojenga utukufu na kujiona, kujisikia na kuwatelekeza wanyonge na masikini. Mifumo ya kujenga umoja na undugu, ya kuishi na kutenda haki, wema na huruma.

Mifumo ya namna hii, inajengwa kwa matendo zaidi ya waraka. Inahitaji kuambukiza na kushawishi.

Yesu, hakufanya miujiza kujionyesha, bali alikuwa na lengo la kuwasaidia watu, kuwatoa katika mateso ya umaskini, kunyanyaswa na kupuuzwa.

Aliponya kwa vile aliwahurumia watu. Alitanguliza huruma, badala ya kutanguliza umaarufu na kuheshimika, alitanguliza wema badala ya kutumia vipaji vyake kujitajirisha na kujineemesha.

Kitu kingine kinachomtofautisha Yesu na manabii wengine na hata Yohana Mbatizaji, ni kwamba Yohana Mbatizaji aliwahubiria wakosaji, alitaka watubu na kumgeukia Mungu. Lakini, Yesu alikwenda kuishi na ombaomba, watoza ushuru na malaya. Mbali na kazi ya kuhubiri, aliishi na kushiriki maisha ya wafuasi wake.

Katika jamii yenye matabaka, mambo mengi yanatumika kuwatenga watu. Miiko inakazaniwa na kuzingatiwa. Kitu kama chakula, kinatumika kama njia ya kuwatenganisha watu, maana huwezi kula chakula na mtu ambaye hayuko kwenye tabaka lako.

Ninakumbuka nikiwa mtoto mdogo, tulikuwa haturuhusiwi kula chakula na wakimbizi kutoka Rwanda au wapagazi kutoka Burundi.

Mtu wa ukoo wa kifalme hakushiriki chakula na watu wa kawaida. Kule Israeli, chakula ilikuwa ni ishara ya urafiki na undugu. Hata kwa ukarimu wa aina gani, mtu hakukuruhusiwa kula chakula au kunywa kinywaji na mtu asiyekuwa wa tabaka lake.

Yesu alivunja miiko hii yote. Alijichanganya na makundi yote, alikula nao, alikunywa nao na kulala kwenye nyumba zao.

Haya yalikuwa mapinduzi makubwa. Yesu hakutofautisha kuhubiri na kuishi maisha ya kila siku na wanajamii. Alitaka kuwaambukiza na kuwashawishi kwa kuishi nao zaidi ya kuwahubiria na kuwaandikia waraka. Alitaka kujenga mfumo wa kuwasaidia watu kuyaishi maisha ya siku kwa siku.

Hapa tunaweza kulinganisha na wahubiri wa leo na maisha ya Kanisa la leo. Watu wanasali pamoja kanisani, lakini wengine wakirudi majumbani kwao wanalala njaa wakati wengine wana chakula cha kula na kusaza. Wengine wanalala kwenye majumba ya kifahari wakati wengine hawana mahali pa kulala.

“Usharika” unabaki kwenye kitendo cha kusali pamoja. Si kushiriki maisha, bali kushiriki sala. Mapadri na wachungaji wanahubiri kama Yohana Mbatizaji, wanahubiri lakini hawajichanganyi na watu.

Mfano wa mifumo

Wanaishi kwenye majumba ya parokia, kwenye nyumba nzuri na kula chakula kizuri tofauti na maisha ya kila siku ya waumini. Jumuiya ya Mkamilishano, iliyokuwa imeanzishwa na Askofu Christopher Mwoleka (marehemu) kule Bushangaro Karagwe, iliyokuwa inalenga kujenga jumuiya moja ya Kikristu kwa waumini walei, mapadri, masista na watawa kuishi maisha ya pamoja; kusali pamoja, kufanya kazi pamoja, kulima pamoja, kusomesha watoto pamoja, kula pamoja, kulala nyumba mmoja, ilipigwa vita na kufutwa.

Sababu kubwa ya kuifuta Mkamilishano ni kwamba watu wenye wakfu (mapadre, masista na watawa) walijichanga na walei walikula meza moja, walilala nyumba moja na waliishi kwa kushirikiana kila kitu na walei.

Jumuiya ya Mkamilishano ilikuwa ikilenga kuwachochea mapadri na wahubiri kuishi maisha ya pamoja na waumini. Kwa lengo la kuwaambukiza na kuwashawishi waumini kuishi maisha ya wakfu. Kuishi kama Yesu alivyoishi miongoni mwa watoza ushuru, maskini, ombaomba na malaya hadi kuyabadilisha maisha yao.

Lengo lilikuwa ni kutengeneza mfumo bora wa waumini kuishi vyema maisha yao ya siku kwa siku ambako mtu angeweza kufundisha uchumi, siasa, elimu ya uraia na mengine mengi bila kelele na malumbano yaliyojitokeza kuhusu waraka wa maaskofu.

Katika Jumuiya ya Mkamilishano mtu angeweza kufundisha elimu ya uraia wakati wowote ule bila kusubiri wakati wa sikukuu za Pasaka na Krismasi.

Kila nikitaja “mfumo”, wasomaji wangu wanauliza ni mfumo gani huo? Ni mfumo wa aina ya Jumuiya ya Mkamilishano. Bahati mbaya ilifutwa.

Na walioifuta jumuiya hiyo hawakuwa na njia nyingine zaidi ya kuandika waraka. Wao, sasa hivi wanajua na kutambua kwamba waraka unawaingiza kwenye matata zaidi ya kupitisha ujumbe wao kwenye Jumuiya kama iliyokuwa ya Mkamilishano.

Ndio maana inashangaza kuwasikiliza wakipaza sauti zao kuutetea waraka wakati wakijua kwamba hawana mfumo mzuri wa kutekeleza waraka huo. Malumbano yaliyojitokeza ni ishara tosha kwamba hawana mfumo na wanalazimika kutengeneza mfumo kwanza.

Tatizo kubwa linaloisimbua jamii yetu ni kutokuwa na mfumo unaoeleweka wa kuishi Ukristu, utu wema na maadili mazuri. Mbali na ufisadi, kuna matatizo mengine mengi kama Ukimwi, maadili mabovu, nk.

Kanisa kuwajibishana

Bahati mbaya hadi leo hii hakuna kanisa lenye mfumo wa kuwajibishana, kushauriana, kuelekezana na kujuliana hali. Hakuna mfumo wa kuhojiana, kama ni fisadi Mkristo na tunasali naye, tukafahamu fedha anazipata wapi.

Ukosefu wa mfumo unalifanya kanisa liendelee kuwakumbatia mafisadi. Fedha za mafisadi zimejenga makanisa, zimenunua vifaa vya kanisani, zimewasomesha mapadri na wachungaji, zimenunua chakula cha mapadri na wachungaji.

Kuna habari kwamba mmoja kati ya mafisadi alikuwa akisalia kila siku katika kanisa moja Dar es Salaam, na kila ibada alikuwa akitoa laki tano.

Kwa vile hakuna mfumo wa kuhojiana, hakuna aliyeuliza ni wapi alikuwa akizipata. Kuna habari kwamba kati ya mafisadi kuna aliyelipatia kanisa vifaa vya ujenzi vya benki. Wako wengine wengi bado wanatoa sadaka fedha za ufisadi. Mapadri, wachungaji, maaskofu na waumini wanazipokeana kuzitumia. Hivyo sote tunashiriki ufisadi bila kujua.

Njia pekee ya kupambana na mafisadi na kuikinga jamii yetu na majanga mengine kama umasikini, ujinga, vita na upweke, ni kujenga jumuiya zinazoishi mshikamano.

Maaskofu wetu hawajafanikiwa kututengenezea mfumo wa kuishi utatu mtakatifu. Ndiyo maana bado tunaandamwa na majanga mengi. Kukemea tu hakutoshi. Ni lazima maaskofu wetu wafanye kazi ya ziada. Yesu, alifanya kazi ya ziada; aliuacha Umungu wake na kujifanya mtu; alifundisha kwa matendo na kutembea kijiji hadi kingine; alitengeneza mfumo wa kuacha yote na kuufuata kwa uaminifu hadi kufia msalabani.

Jumuiya za Kikristu tulizonazo sasa, familia za Kikristu tulizonazo, ambazo zinatishiwa na ugonjwa wa Ukimwi na hatari nyinginezo kama ufisadi ni zile ambazo kila mtu yuko kivyake.

Hakuna anayemchunga, kumlinda na kumwajibisha mwenzake. Kila mtu amejifungia katika nafsi yake. Hakuna uwazi, kufunuliana, kushirikishana, kuchukuliana, kulindana wala kuchungana katika familia wala jumuiya zetu.

Kila mtu anaufunga moyo wake na kubaki na siri nyingi ndani ya nafsi yake. Hata mambo ya kawaida kama kupenda yanafanywa siri. Mambo kama tamaa, uchu, furaha, huzuni yanabaki siri ndani ya moyo wa mtu.

Kuna mafisadi ambao hata wake zao hawafahamu ufisadi wao, ndugu, jamaa na marafiki wanasikia kila kitu kwenye magazeti.

Kuna waandishi wengi, mfano kama Elieshi Lema (Parched Earth) wameandika juu ya tabia hii ya mtu kujifunga ndani ya nafsi yake. Mtu anayeufunga moyo wake hawezi kufanikiwa kutengeneza familia ya kuishi mshikamano wa kimungu. Na kama hakuna familia za kutengeneza mshikamano wa kimungu, ni vigumu kuwa na Jumuiya zenye kuishi mshikamano wa kimungu.

Bila kuwa na Jumuiya zenye kuishi mshikamano wa kimungu, ni lazima tuandamwe na majanga mengi. Ni lazima tuwe na mfumo imara na wa kudumu kuweza kuyakabili majanga yanayoweza kutukumba kimwili na kiroho.

Baba ajifunue kwa mama, na mama vivyo hivyo. Kwa njia hii wanaweza kulindana, kuchungana, kuchukuliana na kusaidiana.

Ni katika uwazi na kufunuliana familia inaweza kuungana na kuwa kitu kimoja. Wazazi wataweza kujenga mfumo wa kuwalinda na kuwachunga watoto wao. Watoto watafundishwa maadili mema, watakua katika uwazi na kutembea katika mwanga.

Familia zilizoungana na kuwa kitu kimoja, zinatengeneza jumuiya iliyoungana ambayo ni lazima pawepo kufunuliana, kujaliana, kulindana, kuchungana na kusaidiana.

Jumuiya ya namna hiyo, ndiyo inayoweza kupambana na majanga makubwa kama ufisadi, rushwa, kutowajibika na Ukimwi. ( soma “The Church as a Family”) cha Marehemu Askofu Christopher Mwoleka:

Hivyo maaskofu wetu wasipige kelele tu, bali watujengee mifumo ya kuuishi Ukristu na maadili mema. Mifumo haiwezi kujengwa na waraka; itajengwa na maisha yenyewe.

Lengo la makala yangu

Lengo zima la makala haya si kuupinga waraka wa maaskofu. Tunataka kuwakumbusha watawala wetu hawa kwamba kuna mambo ya muhimu sana katika jamii yetu zaidi ya ufisadi, demokrasia na uhuru wa maoni. Kama wanataka kutoa mchango wao katika kulijenga taifa letu, basi watutengenezee mfumo mzuri wa kuishi duniani humu kama watoto wa Mungu!

Padri Privatus Karugendo.

+255 754 633122