Watanzania tuna mambo mengi ya kujifunza. Jinsi tunavyowatafuta wataalamu wa uchumi, soko huria na utandawazi kuja kutufundisha, ndivyo tunavyolazimika kuwatafuta wataalamu wa demokrasia, siasa za vyama vingi na uraia kuja hapa kutufundisha.

Tunasema kwamba dunia sasa hivi ni kijiji kimoja. Mambo yanayokijenga na kukiendesha kijiji tunamoishi ni mapya kwetu. Hivyo hatuwezi kukwepa kujifunza mambo hayo.

Ukiyatafakari kwa makini, na hasa kama baadhi hayaendani na sera, dira na maono yako, utayaita ya utapeli. Wataalamu wa mambo haya mapya utawapachika jina la matapeli, wengine siku hizo wanasema mabeberu.

Nimesikia watu wakitoa maoni kwamba tunaweza kuwa na Muungano wa aina yetu bila kuangalia nchi nyingine zinaendesha vipi serikali za muungano na kuwa si lazima Katiba yetu ifanane na nyingine.

Wenye mawazo haya watakuwa wanaogopa utapeli ulio nyuma ya shinikizo lolote lile la mabadiliko yasiyoendana na matakwa ya Watanzania.

Katika mengi tunayopaswa kujifunza hatuwezi kukwepa kuwategemea wataalamu wa nje. Tuna ya kujifunza juu ya dini, utamaduni mpya, utandawazi, soko huria, demokrasia, uraia, vyama vingi vya kisiasa na haki za binadamu.

Tuna mengi ya kujifunza juu ya kutengeneza katiba inayosimamia maslahi ya taifa zaidi ya miaka 100 ijayo; ambayo si ya chama chochote cha siasa; ambayo ikisema serikali mbili, hakuna atakayekaa pembeni na kusema hiyo ni katiba ya CCM, au ambayo ikisema serikali tatu, hakuna atakayekaa pembeni na kusema hiyo ni katiba ya vyama vya upinzani.

Tunapaswa kujifunza kwamba uchu wa madaraka ni mauti; tunashuhudia vita ya uchu wa madaraka nchi za Sudan ya Kusini na Afrika ya Kati; pia tumeshuhudia vita ya uchu wa madaraka kwenye nchi mbalimbali za Afrika.

Nimeshuhudia kijijini kwetu watu waliojenga uhasama mkubwa kati yao kwa vile wako kwenye vyama viwili tofauti CCM na CUF. Ni uhasama wa kutosalimiana, kutokujuliana hali na kutokusaidiana. Sasa hivi Republican na Democrat kule Amerika, wanacheka na kufurahia mipango ya maendeleo na usalama wa nchi yao. Sisi tofauti ya vyama ni uadui wa kudumu! Ni lazima kujifunza.

Tumesikia vitisho wanavyopata wakuu wa wilaya kwamba atakayeachia jimbo kwenda kwenye upinzani atakipata cha moto au jinsi viongozi wa serikali wasivyovumilia maoni tofauti.

Wafanyakazi wa serikali wanakuwa waangalifu kutoonyesha mapenzi yao kwa chama chochote cha siasa zaidi ya CCM. Wakionyesha mapenzi yao kwa upinzani wanakuwa shakani kupoteza kazi. Je, tukiomba msaada wa mafunzo ya siasa ya vyama vingi kutoka kwa watu ambao demokrasia na vyama vingi vya kisiasa ni jadi yao utakuwa ni utapeli?

Demokrasia si jadi yetu. Sisi tulizoea utemi. Leo hii katika kijiji cha utandawazi, utemi hauna nafasi. Ni lazima watu wachague viongozi wao, ni lazima watu wapate nafasi ya kutoa maoni yao. Ni lazima wananchi washirikishwe. Ni lazima watu wawe na uhuru wa kusema ndiyo au hapana – ndiyo maana tunahitaji wataalamu wa kutufundisha.